WINGA machachari wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa, amesema kuwa haikuwa kazi rahisi kwa walichofanya jana walipoichapa Esperance ya Tunisia mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Farid, 19, alikuwa katika kiwango bora jana akifunga bao la kusawazisha dakika ya 69 lililowarudisha mchezoni Azam FC na kupata bao la ushindi ndani ya dakika moja lililofungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ dakika ya 70.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Farid alisema kuwa haikuwa kazi rahisi na wamepambana kinoma kutokana na Esperance kuwa na uzoefu mkubwa kwenye michuano hiyo na pia ukizingatia wamewaacha mbali kisoka.

“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kucheza vema leo (jana) na kuifungia bao timu yangu, haikuwa kazi rahisi kufanya hivyo tumepambana sana hadi kupata matokeo hayo,” alisema.

Azam FC ina nafasi Tunis

Farid alizungumzia pia mchezo wa marudiano utakaofanyika Aprili 20 mwaka huu jijini Tunisia na kudai kuwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri ugenini.

“Bado nina uhakika wa asilimia 100 kwa Azam FC kufanya vizuri ugenini, na hii itawezekana kama watu watajituma kama tulivyojituma hapa kipindi cha pili, vilevile kupeana moyo naamini tutafanikiwa,” alisema.