KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jioni ya leo imefanya kweli baada ya kuidungua Esperance ya Tunisia mabao 2-1 katika mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Mashujaa wa Azam FC leo walikuwa ni viungo washambuliaji Ramadhan Singano ‘Messi’ na Farid Mussa, walioiweka kwenye wakati mgumu ngome ya ulinzi ya Esperance hususani katika kipindi cha pili cha mchezo huo.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ililazimika kutoka nyuma kwa bao moja baada ya Esperance kutangulia kufunga dakika ya 33 kupitia kwa Haithem Jouini aliyepiga kichwa kufuatia krosi ya Iheb Mbaarki.

Kama washambuliaji wa Azam FC nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Tchetche, wangekuwa makini kipindi cha kwanza kwa kuzitumia nafasi nzuri walizozipata, timu hiyo ingeweza kwenda mapumziko ikiwa na uongozi wa takribani mabao 4-1.

Hivyo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Esperance ilikuwa mbele kwa bao hilo, ambapo Azam FC ilirejea kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya kuingia kiungo Frank Domayo ‘Chumvi’ na kutoka Michael Bolou.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Azam FC, ambayo ilianza kucheza soka la kasi kwa kulishambulia mfululizo lango la Esperance kupitia kwa nyota wake wenye kasi Messi, Farid na Tchetche, ambao walikuwa wakichezeshwa vema na viungo Domayo na Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’.

Dakika ya 65 almanusura beki Aggrey Morris aisawazishie Azam FC baada ya kupanda mbele kusaidia mashambulizi na kupiga shuti kali umbali wa takribani mita 35 na mpira kumponyoka kipa wa Esperance, Moez Cherifia, lakini hakukuwa na mmaliziaji karibu jambo ambalo lilimpa urahisi kipa huyo kuuwahi mpira huo na kuudaka tena.

Baada ya jitihada nyingi za kusaka mabao, hatimaye dakika ya 69, Azam FC ikapata bao la kusawazisha lililofungwa kiustadi na Farid, ambaye aliambaa na mpira ndani ya eneo la 18 na kupiga shuti la kiufundi baada ya kupokea pasi safi ya Messi,

Dakika moja baadaye Messi akaipatia bao la pili Azam FC upande ule ule kulia kwa shuti la chini akiunganisha vema krosi iliyochongwa upande wa kushoto na Farid, ambayo ilimpita Bocco kabla ya kujaa kwenye guu la winga huyo aliyeujaza mpira huo wavuni.

Mabingwa hao wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) walilazimika kufanya mabadiliko dakika ya 89 baada ya kuumia kwa beki Pascal Wawa na nafasi yake ilichukuliwa na beki mwenye mwili mkubwa David Mwantika na hadi dakika 90 zinamalizika, Azam FC iliondoka kifua mbele kwa ushindi huo.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kuendeleza rekodi yake nzuri ya kutofungwa mchezo wowote kwenye michuano ya Kimataifa ndani ya uwanja wa nyumbani (Azam Complex) tokea ilipoanza kuutumia kwa michuano hiyo mwaka juzi.

Kihistoria Azam FC ilianza mwaka juzi kwa kuifunga Ferroviario de Beira ya Msumbiji bao 1-0, lililofungwa na Kipre Tchetche katika mchezo wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho, kabla ya kwenda kutolewa ugenini kwa kufungwa 2-0.

Mwaka jana ikawalaza ndani ya uwanja huo vigogo wa Sudan, El Merreikh mabao 2-0 (Didier Kavumbagu, John Bocco) katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ikatolewa baada ya kupigwa 3-0 jijini Khartoum, Sudan.

Mwaka huu imewapiga Bidvest Wits mabao 4-3 na kuvuka hadi raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi wa jumla ya mabao 7-3 kufuatia kuibuka na ushindi wa 3-0 katika Uwanja wa Bidvest, jijini Johannesburg na leo hii imeibabua Esperance 2-1.

Azam FC inahitaji ushindi wowote au sare yoyote katika mchezo wa marudiano uliopangwa kufanyika Aprili 20 jijini Tunis, ili iweze kuitoa Esperance na kutinga hatua ya mwisho ya mtoano kwa kucheza na moja ya timu iliyotolewa kutoka Ligi ya Mabingwa ya Afrika kabla ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali (hatua ya makundi) ya michuano hiyo.

Kwa mujibu wa malengo iliyojiwekea Azam FC kabla ya kuanza msimu huu ni kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kutofikia mafanikio hayo kwa miaka mitatu iliyopita tokea ianze kushiriki mashindano ya Afrika.

Kikosi Azam FC leo:

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Wazir Salum/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk 67, Aggrey Morris, Pascal Wawa/David Mwantika dk 89, Jean Baptiste Mugiraneza, Kipre Tchetche, Kipre Bolou/Frank Domayo dk 46, Ramadhan Singano ‘Messi’, John Bocco na Farid Mussa.