KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kesho Jumapili itarusha karata yake ya kwanza muhimu kwenye raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, pale itakapowakaribisha Esperance ya Tunisia katika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ipo fiti kabisa kuelekea mchezo huo, lakini itaingia dimbani ikiwa bila nyota wake wawili beki Shomari Kapombe na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambao ni wagonjwa.

Kapombe hivi sasa bado yupo nchini Afrika Kusini akiendelea na vipimo kwa ajili ya kubaini tatizo linalomsumbua kutokana na kubanwa mbavu huku Sure Boy akisumbulia na mjeraha ya nyonga aliyoyapata wakati wa mchezo wa Ndanda.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema licha ya kuwakosa nyota wake hao amejipanga kuja na mfumo mpya utakaowawezesha kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Esperance.

“Nitawakosa Sure Boy na Kapombe kwenye mchezo wa kesho, Sure Boy anahitaji mapumziko ya siku nne ili kurejea kwenye hali yake ya kawaida, kwa Kapombe bado haijajulikana kwani hivi sasa tunasubiria ripoti kutoka Afrika Kusini kujua maendeleo ya afya yake.

“Nitakuja na mfumo mpya kwa ajili ya kupambana na hali hiyo ambao utaanza tukiwa na mabeki wanne ambao utakuwa ni mzuri wa kupambana na mfumo wa 4-2-3-1 wanaotmia wapinzani wetu, hivyo mabeki wa pembeni wataanza Erasto Nyoni na Wazir Salum, pengo la Sure Boy litazibwa na Messi (Ramadhan Singano), atakayecheza kama namba 10,” alisema.

Hall alisema amelenga ushindi kwenye mchezo huo na kudai kuwa atapanga kikosi chenye muonekano wa kushambulia zaidi kwenye nafasi za mbele ukiondoa viungo wawili wa ukabaji watakaokuwa wakiwasaidia mabeki kutimiza majukumu ya kukaba.

Mfanano wa timu hizo   

Timu hizo zinakutana wakati zikiwa na mfanano wa nafasi katika ligi zao, wakati Azam FC ikiwa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa kujikusanyia jumla ya pointi 52, Esperance nayo ipo nafasi hiyo ndani ya Ligi Kuu Tunisia baada ya kujizolea pointi 51.

Mpaka zinafikia raundi ya pili ya michuano hiyo, timu hizo zimepanya raundi hiyo baada ya kupata ushindi mnono kwenye mechi za raundi ya kwanza walipoanzia, Azam FC ikiitoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 7-3 huku Esperance nayo ikiifurusha nje Renaissance ya Chad kwa ushindi wa 7-0.

Rekodi ya Azam FC (Azam Complex)

Azam FC bado ina rekodi nzuri kila inatumia uwanja wake wa nyumbani kwani mpaka sasa kwenye michuano yote ya kimataifa haijawahi kufungwa ndani ya dimba hilo tokea waanze kuutumia kwa mechi hizo mwaka juzi.

Mabingwa hao wa michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki Kati (CECAFA Kagame Cup), walianza mwaka juzi kwa kuifunga Ferroviario de Beira ya Msumbiji kwa bao 1-0 lililofungwa na Kipre Tchetche katika mchezo wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho, kabla ya kwenda kutolewa ugenini kwa kufungwa 2-0.

Mwaka jana ikawalaza vigogo wa Sudan, El Merreikh, kwa jumla ya mabao 2-0 (Didier Kavumbagu, John Bocco) katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ikatolewa baada ya kupigwa 3-0 jijini Khartoum, Sudan.

Mwaka huu ikailaza Bidvest Wits mabao 4-3 na kuvuka kwa ushindi wa jumla ya mabao 7-3 kufuatia kuibuka na ushindi wa 3-0 katika Uwanja wa Bidvest, jijini Johannesburg, hivyo kesho Azam FC itakuwa na kila sababu ya kutaka kuendeleza rekodi yake hiyo bora.

Viingilio Azam FC v Esperance

Mashabiki wa soka nchini wamerahisisha kabisa kushuhudia mchezo huo utakaokuwa mkali na wa aina yake, kwani ili uweze kushuhudia uhondo huo itakugharimu kiasi kiduchu tu cha Sh. 5,000 kwa majukwaa ya mzunguko.

Kwa majukwaa ya watu maalumu (VIP), kiingilio cha VIP A kitakuwa ni Sh. 20,000 tu huku VIP B kikiwa ni Sh. 10,000, ambapo tiketi zote hizo zitapatikana kuanzia kesho saa 3.00 asubuhi kwa kuuzwa kwenye Ukumbi wa Dar Live Mbagala Rangi Tatu na kituo kingine kitakuwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam itakapofanyika mechi hiyo.