MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Kipre Tchetche, ameingia kwenye orodha ya wachezaji wanne wanaofukuzia ufungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.

Tchetche ameingia kwenye orodha hiyo baada ya kufunga mabao matatu wakati Azam FC ikiichapa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa pili wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo walipoichapa 4-3 na kufuzu raundi ya pili kwa ushindi wa jumla wa 7-3.

Mabao hayo yalimfanya mshambuliaji huyo kutoka Ivory Coast kuandika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga ‘hat-trick’ mwaka huu ndani ya michuano hiyo, ambayo kuanzia kesho itafungua dimba kwa mechi za raundi ya pili.

Mchezaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/14 Azam FC ilipotwaa ubingwa wa ligi hiyo bila kufungwa mchezo wowote, amelingana kwa mabao na washambuliaji wengine wawili ndani ya michuano hiyo kila mmoja akiwa ametupia wavuni mabao matatu.

Wachezaji hao aliokabana nao koo ni Amr Barakat anayekipiga Misr El-Makasa ya Misri pamoja na straika kutoka Harare City ya Zimbabwe, Raphael Manuvire, ambaye ndiye pekee timu yake imetolewa kwenye raundi ya kwanza.

Nyota hao wenye mabao matatu kwa pamoja wanamfukuzia straika Arsénio Sebastião Cabúngula ‘Love’, anayekipiga katika timu ya Sagrada Esperança kutoka nchini Angola, ambaye ndiye kinara wa mabao akiwa ameshatupia mabao manne mpaka sasa.

Tchetche ana nafasi ya kuwakimbiza na kuwapa presha wapinzani wake hao kwenye mbio hizo za ufungaji bora kama ataendeleza kasi yake ya upachikaji mabao kwa kutupia mabao, wakati Azam FC itakapoikaribisha Esperance ya Tunisia keshokutwa Aprili 10 katika mchezo wa raundi ya pili ya michuano hiyo na pia ule wa marudiano utakaopigwa Aprili 20 jijini Tunis.