BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, ameondoka nchini leo saa 9.35 Alasiri akielekea Afrika Kusini kwa ajili ya kutibiwa kifua ambacho kinamsumbua.

Kapombe aliyekosa mechi mbili zilizopita za Azam FC dhidi ya Toto Africans na Ndanda, alianza kuumwa na kifua wakati kikosi hicho kikijiandaa kuvaana na Toto jijini Mwanza kabla ya kukimbizwa hospitalini.

Awali beki huyo alikuwa akisumbuliwa na homa kali ya mafua ambayo pia iliwaathiri baadhi ya wachezaji wa Azam FC waliotoka nchini Chad kwenye kambi ya Taifa Stars akiwemo nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na hiyo ni kutokana na hali mbaya ya hewa iliyoko jijini N’Djamena.

Kapombe ameelekea nchini humo sambamba na Daktari wa timu, Dr. Juma Mwimbe, ambapo mara baada ya kuwasili kesho wataelekea kwenye Hospitali ya Morningside Mediclinic iliyopo jijini Johannesburg kwa ajili ya beki huyo kuanza kufanyiwa vipimo ili kubainika tatizo.

“Kapombe anasikia maumivu ya kifua na mara kwa mara amekuwa akilalamika mbavu zinamuuma, tunashukuru Mungu kwa sasa hali yake inaendelea vizuri tofauti na awali, ila tunachoenda kufanya huko ni kuangaliwa zaidi ni kinamsumbua kwa kuchukuliwa vipimo na baadaye ndio itajulikana kitaalamu ni kinamsumbua,” alisema Mwimbe wakati akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz dakika chache kabla hawajaelekea huko na ndege ya Shirika la Afrika Kusini.

Beki huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa, amekuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa Azam FC msimu huu kwenye mechi mbalimbali alizocheza, akiwa mpaka sasa amefunga jumla ya mabao 11 kwenye michuano yote, nane katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Mabao mengine mawili amefunga kwenye Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) huku moja akifunga katika Kombe la Shirikisho Afrika (CC) dhidi ya Bidvest Wits walipoichapa 3-0 jijini Johannesburg kabla ya kufuzu raundi ya pili ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 7-3 na sasa itakutana na Esperance de Tunis Jumapili ijayo (Aprili 10) na mchezo wa marudiano jijini Tunis Aprili 20.