SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeweka hadharani waamuzi watakaochezesha mechi mbili za raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC na Esperance de Tunis.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAF, inaonyesha kuwa mchezo wa kwanza baina ya timu hizo utakaofanyika Aprili 10 Jumapili hii ndani ya Uwanja wa Azam Complex kwa wenyeji Azam FC kuwakaribisha waarabu hao, itachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Afrika Kusini.

Mwamuzi wa kati anatarajia kuwa Daniel Frazer Bennett, 40, ambaye mwaka jana alichezesha mchezo wa pili wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Esperance na El Merreikh ya Sudan ambao Watunisia hao walishinda mabao 2-1 jijini Rades, lakini walitolewa kwa sheria ya bao la ugenini baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Khartoum kuisha kwa Merreikh kushinda bao 1-0.

Waamuzi wasaidizi kwenye mchezo huo wanatarajia kuwa Zakhele Thusi Siwela (mwamuzi msaidizi namba moja) na mwamuzi msaidizi namba mbili ambaye ni Thembisile Theophilus Windvoel.

Mchezo wa marudiano utakaofanyika Aprili 20 kwenye Uwanja wa Stade Olympique De Rades jijini Rades, Tunisia, utachezeshwa na waamuzi waarabu kutoka Morocco, mwamuzi wa kati akiwa ni Rédouane Jiyed, Mouhib Abdallah Filali (mwamuzi msaidizi namba moja) na Essam Benbapa (mwamuzi msaidizi namba mbili).