KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, inatarajia kushuka dimbani kesho saa 10.30 jioni kuikaribisha Ndanda katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam FC itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo uliopita dhidi ya Toto Africans ya Mwanza, uliopigwa ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza Jumapili iliyopita na kuathiriwa na mvua kubwa iliyonyesha kabla ya kuanza na wakati mechi hiyo ikiendelea.

Ndanda yenyewe nayo imetoka kulazimishwa suluhu kwenye mchezo uliopita dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, uliofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Azam FC itaimarika kesho baada ya urejeo wa mshambuliaji Kipre Tchetche aliyepona majeraha ya enka aliyopata wakati akipiga hat-trick walipoichapa Bidvest Wits ya Afrika Kusini mabao 4-3.

Alichosema Stewart Hall                 

Mabingwa hao Kombe la Kagame wanaodhaminiwa na Benki ya NMB, wamelenga kurejea kwenye hali yake ya kawaida kwa kuichapa Ndanda, ili kuendelea kuwapa presha wapinzani wake Yanga na Simba katika mbio za ubingwa huo.

Akizungumza mapema na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz  wakati kikosi hicho kiliporejea jijini Dar es Salaam kikitokea jijini Mwanza, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa ni lazima washinde mchezo huo ili kuendelea kuwa kwenye mbio za ubingwa kwani kwa mujibu wa mahesabu bado wana nafasi kubwa ya kuubeba.

“Utakuwa ni mchezo mgumu kwani tunajua kuna baadhi ya watu wataipa fedha Ndanda ili iweze kutuzuia sisi kwa kucheza soka la kujilinda zaidi, hivyo sisi tumejipanga na tunajua namna ya kuzuia mbinu zao hizo,” alisema.

Rekodi (Head to Head)

Mpaka sasa Azam FC imekutana mara tatu na Ndanda kwenye mechi za ligi, ikishinda mara mbili (1-0, 1-0) moja ndani ya Uwanja wa Azam Complex na nyingine Nangwanda huku ikipoteza mmoja (1-0) uliofanyika Mtwara Novemba Mosi mwaka juzi.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza uliofanyika Mtwara, Azam FC iliibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo mgumu ambao ushindi huo uliamuriwa dakika za mwisho na beki Shomari Kapombe, alipiga bao kwa kichwa akiunganisha krosi ya Kipre Tchetche.

Msimamo VPL

Azam FC mpaka sasa imejikusanyia jumla ya pointi 51 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, nyuma ya Yanga iliyojikusanyia 53 huku Simba iliyocheza michezo miwili zaidi dhidi ya timu hizo ikiwa kileleni kwa pointi 57.

Katika mechi 22 za ligi ilizocheza hadi sasa, Azam FC imeshinda mechi 15, sare sita na kufungwa mchezo mmoja dhidi ya Coastal Union (1-0) huku ikifunga jumla ya mabao 38.

Ushindi wowote wa Azam FC kesho utaifanya kufikisha jumla ya pointi 54 na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa kuishusha Yanga, lakini wakiwa wameizidi mchezo mmoja wa kucheza.

Ndanda iliyopanda daraja msimu uliopita yenyewe ipo katika nafasi ya 11 kwa pointi 26 ilizojikusanyia, ndani ya michezo 24 waliyocheza wameshinda mara tano, sare 11 na imefungwa mara nane huku ikitupia mabao 20.