KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imeanza kazi ya kujiandaa kisayansi kuelekea mchezo wa hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance de Tunis ya nchini Tunisia.

Azam FC itaanza kucheza na miamba hiyo nyumbani Aprili 10 mwaka huu kabla ya kuelekea jijini Tunis kwa ajili ya mchezo wa marudiano, ambao utatoa mshindi wa jumla wa kupenya hadi hatua ya mwisho ya mchujo na kutinga hatua ya robo fainali (makundi).

Uongozi wa Azam FC katika kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi zote mbili, tayari Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Saad Kawemba na Kocha Msaidizi, Dennis Kitambi, wapo jijini Tunis kuwasoma wapinzani wao hao, ikiwemo kuandaa mazingira watakapofikia wachezaji pindi timu itakapowasili nchini humo kwa mchezo wa marudiano.

Kama hiyo haitoshi leo jioni walikuwepo uwanjani kushuhudia ‘live’ mechi ya Esperance waliokuwa wakipambana na mahasimu wao, Club African iliyofanyika Uwanja wa Stade Olympique De Rades unaotumiwa na Esperance, ambao wameibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Mbali na kuangalia mchezo huo, tayari benchi la ufundi la Azam FC limepata DVD za mechi zilizopita na wamefanya hivyo ili kuwaandaa wachezaji kimbinu kwa ajili ya kumenyana vema na waarabu hao.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB imejiwekea malengo ya kufika robo fainali ya michuano hiyo, ambapo imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-3.

Esperance yenyewe imesonga mbele baada ya kuichapa Renaissance ya Chad kwa jumla ya mabao 7-0.