KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC kipo fiti kabisa kuivaa Toto Africans kesho Jumapili huku wachezaji wakiwa na morali kubwa ya ushindi katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Kirumba, Mwanza kuanzia saa 10.00 jioni.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, jioni ya leo imefanya mazoezi ya mwisho kabisa kabla ya kukabiliana na Toto, ambapo wachezaji wameonyesha hali ya kupambana muda wote jambo ambalo linaonyesha kuwa wapo tayari kuzoa pointi zote tatu kesho.

Wakati hali ikiwa hivyo, kuelekea mchezo huo Azam FC itamkosa Shomari Kapombe, aliyefunga mabao nane mpaka sasa Ligi Kuu msimu huu na hiyo ni baada ya beki huyo kisiki wa kulia kutokuwa katika hali nzuri kiafya kufuatia kuendelea kusumbuliwa na homa kali ya mafua na safari hii ikiwa imeambatana na kifua.

Kapombe aliyeshindwa kufanya kabisa mazoezi leo, jana usiku alikimbizwa hospitali baada ya kutojisikia vema, na kwa mujibu wa jopo la kitabibu la Azam FC chini ya Daktari Juma Mwimbe, limesema kuwa asilimia kubwa ya wachezaji wa timu hiyo waliokuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars wamepatwa na ugonjwa wa mafua kutokana na hali mbaya ya hali hewa ya joto nchini Chad walipokwenda kucheza na Taifa hilo.

Baadhi ya wachezaji wengine wa Azam FC waliokumbwa na homa hiyo ya mafua ni nahodha John Bocco ‘Adebayor’, kipa Aishi Manula, David Mwantika, ambao kwa sasa hali zao kiafya ziko vizuri.

Habari njema kuelekea mtanange huo ni kurejea kwa mshambuliaji hatari wa kikosi hicho, Kipre Tchethe, aliyekuwa akiuguza majeraja ya enka aliyopata wakati Azam FC ikiibanjua Bidvest Wits ya Afrika Kusini mabao 4-3 huku Tchetche akipiga hat-trick.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica, alisema wana nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo wa kesho Jumapili huku akigusia kuwa mbali na Kapombe, ambaye ataukosa mchezo huo pia kuna baadhi ya wachezaji wana majeraha madogo.

“Tunajiamini ya kuwa tutaendelea kupata matokeo mazuri tuliyopata katika mechi zilizopita kwa kushinda kesho, Toto Africans ni timu nzuri wanacheza mpira mzuri, hivyo tunatarajia upinzani mkali, lakini tunaamini ya kuwa tuna kikosi kizuri cha kupambana na hilo,” alisema.

Azam FC v Toto (Head to Head)

Mabingwa hao wa Kombe la Kagame wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga timu hiyo mabao 5-0 kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi, mechi iliyofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Ukiachana na hilo, kihistoria mpaka sasa timu hizo zimekutana mara saba kwenye mechi za ligi, Azam FC ikishinda mechi nne, Toto mbili na moja ikiisha kwa sare.

Ndani ya mechi hizo saba, jumla ya mabao 17 yamefungwa, Azam FC ikiwa imefunga robo tatu ya mabao hayo (13) na Toto Africa ikiambulia kugusa nyavu za wapinzani wake hao mara nne tu.

Mpaka sasa kwenye msimamo wa ligi hiyo, Azam FC inashika nafasi ya tatu ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi 50 sawa na Yanga iliyo nafasi ya pili, Toto yenyewe ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 26.

Matokeo mechi zilizopita;     

04-11-2015   Azam FC  5-0 Toto Africa

04-02-2011   Azam FC  3-0 Toto Africa

18-09-2010  Toto Africa 1-0 Azam FC

26-01-2010  Azam FC   1-0 Toto Africa    

27-08-2009  Toto Africa 2-2 Azam FC

26-04-2009  Toto Africa 1-0 Azam FC

24-09-2008  Azam FC   2-0 Toto Africa