BAO alilofunga jana winga wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’ dhidi ya Tanzania Prisons limemuongezea morali nyota huyo katika kuongeza juhudi ya kutupia mabao zaidi katika mechi zinazokuja.

Vialli aliyeingia dakika ya 60 kuchukua nafasi ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’, alifunga bao hilo kwa juhudi binafsi dakika ya 86 akimpindua beki mmoja wa Prisons, alieyedondoka chini na kupiga shuti la ufundi lililomshinda kipa wa Prisons Beno Kakolanya.

Bao hilo liliihakikishia Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, nafasi ya kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Vialli alisema bao hilo limemkumbusha mbali sana kwenye maisha yake ya soka hasa ikizingatiwa hajafunga bao kwa muda mrefu tokea msimu uliopita.

“Namshukuru Mungu sana kwa kufunga leo (jana), najisikia furaha sana hivi sasa, nimesota muda mrefu kuhangaikia kufunga bao langu la kwanza tokea nitoke kwenye majeraha ya muda mrefu, nashukuru nimetimiza hilo, kwa kweli bao hili limeniongezea morali ya kufunga mabao mengine katika mechi zijazo,” alisema.

Winga huyo machachari aliyehamishiwa kwenye nafasi ya ushambuliaji hivi sasa kupitia mfumo mpya wa 3-5-2, aliongeza kuwa: “Unajua jambo kubwa nililokuwa nikilikosa ni kukosa muda mwingi wa kucheza na hii imechangiwa na majeraha niliyopata msimu uliopita, nashukuru nimeanza kurejea taratibu baada ya ya kufanya mazoezi makali chini ya makocha na mengine ya kwangu binafsi, nimefurahi kwa kweli leo hii.”

Hall afurahishwa

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, naye amefurahishwa sana na kiwango cha Mcha kwenye mchezo huo na kudai kuwa kiwango chake kinazidi kuimarika kadiri siku zinavyokwenda.

“Mcha ameanza kurejea kwenye kiwango chake cha awali, kwa siku za hivi karibuni amekuwa akifanya vizuri mazoezini na hata bao alilofunga leo (jana) limedhihirisha hilo,” alisema.  

Hall pia alisema kikosi chake kimecheza vizuri sana kipindi cha pili mara baada ya kuwaingiza Frank Domayo na Khamis Mcha na hiyo ndio sababu kubwa iliyowafanya kupata mabao mawili yaliyoamua mchezo huo katika kipindi hicho.

“Tunashukuru tumeingia nusu fainali, tunatarajia tutapangiwa Simba au Yanga ndani ya hatua hiyo, yote kwa yote sisi tumejiandaa kwa lolote na mpinzani yoyote tutakayeoangiwa,” alisema.

Mabao mengine ya Azam FC kwenye mchezo huo yalifungwa na beki hatari wa timu hiyo, Shomari Kapombe, aliyefikisha jumla ya mabao 11 msimu huu, akifunga nane kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), mawili katika Kombe la FA na moja ndani ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC).