KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imewasili salama jijini Mwanza ikiwa na ari kubwa ya kuzoa pointi tatu dhidi ya wenyeji wao Toto African katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika ndani ya Uwanja wa Kirumba jijini humo keshokutwa Jumapili (Aprili 3).

Azam FC iliondoka jijini Dar es Salaam saa 9.20 mchana ikiwa na kikosi kamili kasoro beki wa kushoto Gadiel Michael anayeendelea na programu ya kuondoa majeraha yake ya goti yanayomsumbua na imefikia katika Hoteli ya Mipa iliyopo jijini hapa.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz muda mchache kabla ya kikosi hicho akijakwea ndege kuelekea mkoani humo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema wamekwenda na lengo moja tu la kuchukua pointi tatu katika mchezo huo.

“Ligi imefikia sehemu muhimu sana, kukusanya pointi ni jambo la msingi sana, tukishinda mechi zet zote zilizobakia tuna uhakika na ubingwa wa ligi, hivyo tumelenga pointi tatu dhidi ya Toto,” alisema.

Akizungumzia programu watakayoanza nayo jijini hapa kabla ya mchezo huo, Hall alisema watafanya mazoezi kesho ndani ya uwanja huo na wanachosubiria ni kutajiwa muda na wenyeji wao.

Azam FC kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 50 sawa na Yanga iliyo juu yake, lakini timu zote hizo zimezidiwa mechi tatu na Simba inayoongoza ligi kwa pointi 57.