KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kesho saa 10.00 jioni itakuwa na shughuli pevu ya kusaka tiketi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kwa kuvaana na maafande wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Azam FC iliyofanya mazoezi ya makali kujiwinda na mchezo huo, itakuwa ikicheza kwa mara ya kwanza ndani ya uwanja wa nyumbani kwenye michuano hiyo baada ya mechi mbili zilizopita kucheza ugenini katika viwanja visivyokuwa na ubora unaostahili.

Hadi inafika hatua hiyo iliweza kuitoa African Lyon (4-0) katika hatua ya 32 bora kabla ya kuisukuma nje Panone ya mjini Moshi kwa jumla ya mabao 2-1 na sasa itavaana na Prisons ambayo imetoka kuwatoa ndugu zao Mbeya City kwa ushindi wa 2-1.

Rekodi  zao (head to head)

Mara kwa mara timu hizo zinapokuwa zikikutana huonyeshana upinzani mkali, ambapo kwa mujibu wa historia zimekutana mara 12 kwenye michezo mbalimbali ya ligi na hii ni mara ya kwanza kukutana ndani ya Kombe la FA.

Kitakwimu kwenye mechi hizo 12 za ligi, rekodi inaonyesha kuwa mpaka sasa timu hizo ziko sawa, kwani wote wameenda sare mechi tano na kila mmoja kushinda mara tatu, na cha kustaajabisha kabisa katika mabao 20 yalifungwa ndani ya mechi zote, kila timu imefunga mabao 10.

Jumla ya mabao 20 yamefungwa na timu hizo katika idadi hiyo ya mechi, cha kustaajabisha zaidi kila timu imefunga mabao 10 jambo ambalo linaongeza zaidi mvuto wa mchezo wa kesho.

Ikumbukwe ya kuwa Azam FC inayodhaminiwa na Benki bora kabisa ya NMB, itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Prisons mabao 2-1 ndani ya dimba hilo kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi, mabao yaliyowekwa kambani na Kipre Tchetche na Farid Mussa.

Kauli ya Stewart Hall

“Tunaijua Prisons ni timu ngumu na inayotumia nguvu sana, tunafikiria ya kuwa watakuja na mbinu ya kuzuia zaidi kama walivyofanya tulivyocheza nao Mbeya na kutoka sare, kwani watakuwa na furaha ya kufika katika penalti.

“Hivyo sisi kwa upande wetu tunatakiwa kuwa bora na kuharibu mbinu zao hizo, sisi tutacheza kwa kushambulia sana ili kupata bao la mapema na kuharibu mbinu walizokuja nazo,” alisema Hall wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz.

Watatu kuikosa Prisons   

Hall ameweka bayana kuwa kuelekea mchezo huo anatarajia kuwakosa wachezaji watatu, Kipre Tchetche na Gardiel Michael walio majeruhi pamoja na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, ambaye ameugua homa ya mafua.

“Hakuna tatizo kukosekana kwa nyota hao (Bocco, Kipre), bado nina kikosi kipana chenye washambuliaji wengine wanne ambao nitaangalia nani yupo fiti kwa ajili ya kuziba nafasi zao, ila kwa Bocco yeye ataweza kuwa fiti kwa mchezo wa Jumapili (Toto African),” alisema.

Katika hatua nyingine Hall amesema kuwa anatarajia kumpumzisha kiungo Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ aliyetarajiwa kuwasili nchini leo akitoka kuitumikia timu yake ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’.

Migi anapumzishwa baada ya kucheza mechi mbili mfululizo za Rwanda dhidi ya Mauritius, mchezo wa mwisho wakimalizia jana kwa kuishushia mvua ya mabao 5-0 timu hiyo huku kiungo huyo hodari wa ukabaji akitupia bao moja.

“Migi anarudi akiwa amechoka kutokana na majukumu ya timu yake Taifa, nataka kumpumzisha ili awe fiti kwenye mchezo wa Jumapili dhidi ya Toto Africans, pia kuna baadhi ya nyota waliotumikia Taifa Stars nao wameonekana kuwa na uchovu, hivyo baadhi yao nao nitawapumzisha,” alisema.

Mwingereza huyo alimalizia kwa kusema kuwa anakabiliwa na ratiba ngumu ya kucheza mechi nne ndani ya siku 10 na kudai kuwa atapambana na hali hiyo kwa kubadilisha kikosi mara kwa mara (rotation) kadiri itakavyowezekana.

Wakati Azam FC ikiwa imejiwekea malengo makubwa ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeweka wazi kuwa bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC) mwakani.