KIKOSI cha vijana cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam Academy’ inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam saa 2.00 asubuhi Alhamisi ijayo.

Azam FC ni timu pekee nchini iliyofanya uwekezaji mkubwa kwenye soka la vijana kwa kuanzisha kituo cha kulea vipaji ndani ya makao makuu yake Azam Complex, ambayo kwa sasa inafundishwa na Mwingereza Tom Legg na Msaidizi wake, Idd Cheche.

Mbali na baadhi ya wahitimu wa academy hiyo kusambaa kwenye timu mbalimbali nchini, Azam FC ndani ya kikosi chake cha wakubwa imewavuna nyota kadhaa ambao ni kipa bora kabisa nchini kwa sasa Aishi Manula ‘Tanzania One’, mabeki Abdallah Kheri, Gadiel Michael, viungo Mudathir Yahya, Farid Mussa.

Wengine walioko timu kubwa waliotolewa kwa mkopo ni beki Ismail Gambo ‘Kusi’ (Mwadui), viungo Omary Wayne (African Sports), Bryson Raphael (Ndanda), Joseph Kimwaga (Simba) na mshambuliaji Kelvin Friday (Mtibwa Sugar).

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam Academy, Tom Legg, alisema lengo kuu la mchezo huo ni kuiunga mkono Serengeti Boys inayojiandaa kukipiga na Misri katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Jumamosi ijayo.

“Hatuna kingine kikubwa kwenye mchezo huo zaidi ni kuiunga mkono TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), Kim Poulsen (Kocha wa kikosi hicho) na timu kwa ujumla kwani itacheza na Misri Jumamosi, sisi tumejiandaa kuwapa mazoezi mazuri,” alisema.

Seremgeti Boys ipo kwenye maandalizi makali kujiandaa na mchezo wa kwanza wa kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa vijana (U-17) nchini Madagascar 2017 kwa kukipiga na Shelisheli kati ya Juni 24, 25, 26 nchini na marudaino kuchezwa Julai 01, 02, 03 nchini Shelisheli.

Mshindi wa mchezo huo namba 15 na16 atacheza dhidi ya timu ya Taifa ya Afrika Kusini katika hatua inayofuata ya 16 bora, ambayo itatoa timu 8 zitakazofuzu kwa fainali hizo.