KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kimepewa mapumziko ya siku tatu tokea jana kufuatia ligi kusimama kupisha mechi za timu za Taifa za kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani.

Jumla ya wachezaji tisa wa Azam FC wameondoka kujiunga na timu zao za Taifa, saba wakiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ huku kiungo Jean Mugiraneza ‘Migi’ akijiunga na Rwanda ‘Amavubi’ na Didier Kavumbagu akiwa na Burundi ‘Intamba Mu Rugamba’.

Wachezaji wa Azam FC waliojiunga na Stars itakayocheza na Chad jijini D’jamena kesho ni kipa Aishi Manula, mabeki David Mwantika, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, viungo ni Himid Mao ‘Ninja’, Farid Mussa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, ambaye ni nahodha msaidizi wa kikosi hicho.

Kwa mujibu wa programu ya benchi la ufundi la Azam FC, kikosi cha timu kinatakiwa kurejea tena mazoezini keshokutwa Alhamisi saa 2.30 asubuhi kwa wale ambao hawajaitwa katika timu zao za Taifa.

Mara baada ya kuanza mazoezi hayo, Ijumaa ijayo (Machi 25) jioni kutakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Friends Rangers na kwa mujibu wa programu ya mechi hiyo, benchi la ufundi linataka kuutumia mchezo huo kuwaangalia wachezaji ambao hawajapata muda mrefu wa kucheza.

Majeraha ya Kipre Tchetche?

Taarifa zilizotoka kwenye benchi la kitabibu la Azam FC, zinasema kuwa Tchetche hajapata majeraha makubwa kama inavyodhaniwa katika mchezo uliopita dhidi ya Bidvest Wits.

Tchetche alipata majeraha ya enka dakika ya 88 mara baada ya kufunga bao la tatu akimalizia hat-trick yake Jumapili iliyopita dhidi ya Bidvest Wits, majeraha yaliyomfanya kushindwa kuendelea na mchezo huo na Azam FC kulazimika kucheza pungufu ya mchezaji mmoja hadi mpira huo unamalizika.

Akizungumza na mtandao wa rasmi wa klabu hii wa www.azamfc.co.tz Daktari wa Azam FC, Dr. Juma Mwimbe alisema kuwa Tchetche amepata majeraha madogo ambayo hayawezi kumfanya akose mechi zijazo za mabingwa hao wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la CECAFA Kagame).

“Anahitaji kupumzika kwa siku tatu tokea jana na baadaye ndio tutakiwa kumfanyia vipimo ili kuona kama atatakiwa kupumzika kwa muda gani au atatakiwa kuendelea na programu za mazoezi za kawaida, lakini majeraha aliyopata ni madogo hayawezi kumfanya akose mechi zijazo,” alisema.