TIMU ya Azam Veteran jana usiku ilizidi kujikita kileleni kwenye msimamo wa Ligi ya JMK Floodlight baada ya kupewa ushindi wa mezani kufuatia wapinzani wao Copy Catz kuchomekea wachezaji wasiokuwa na umri sahihi.

Michuano hiyo inayofanyika katika kituo cha michezo cha JMK Youth Park, Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, ni maalumu kwa ajili ya timu za maveterani wenye umri kuanzia miaka 30 huku wachezaji watatu tu wakitakiwa kusajiliwa kwa wale waliochini ya umri huo.

Hivyo baada ya waandaaji wa michuano hiyo kupekua leseni za wachezaji wa Copy Catz walibaini ya kuwa ni wachezaji saba pekee waliokidhi vigezo na kutakiwa kuchagua moja, kucheza kwa idadi hiyo kutokana na taratibu za soka kuruhusu au waiachie Azam Veteran izawadiwe mabao matano na pointi tatu kufuatia wao kukiuka taratibu.

Copy Catz ilimaliza mjadala huo kwa kukubali yaishe kwa kugomea kucheza kwa idadi hiyo ya wachezaji na hivyo Azam Veteran ikapata ushindi wa mezani, ulioifanya kufikisha jumla ya pointi 18 kileleni mwa Kundi B.

Mpaka sasa Azam Vetaran imeshacheza jumla ya mechi saba za michuano hiyo ikiwa imeshinda sita na kufungwa mmoja huku ikiwa imebakisha michezo mitatu kabla ya kumaliza hatua ya makundi na kutinga robo fainali.

Yaichapa Soccer City?

Baada ya mchezo huo kuishia hapo huku timu zote zikiwa zimevaa jezi kwa ajili ya kuchuana, Copy Catz pia iliigomea Azam Veteran kucheza mchezo wa kirafiki, ambayo ilikubaliwa kukipiga na Soccer City FC.

Katika mchezo huo wa kirafiki Azam Veteran iliweza kupata ushindi mnono wa mabao 4-1, yaliyofungwa na Abdulkarim Amin ‘Popat’ aliyefunga mawili huku Salim Aziz na Mbaraka Shabaan wakipiga bao moja kila mmoja.