STRAIKA hatari wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Kipre Tchetche, ameweka rekodi ya kufunga hat-trick ya kwanza kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka huu baada ya jana kufunga mabao matatu katika ushindi wa timu hiyo wa 4-3 dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex,Chamazi jijini Dar es Salaam.

Hat-trick hiyo pia imemfanya Tchetche kuweka rekodi nyingine ya kutupia mabao matatu kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Tanzania na michuano ya CAF tokea alipojiunga na Azam FC mwaka 2011 akitokea Jeunesse Club d’Abidjan Treichville (JCAT) ya kwao Ivory Coast.

Kihistoria hiyo ni hat-trick yake ya pili kwenye soka la ushindani, ya kwanza akiifunga alipokuwa JCAT walipocheza na Bingerville (4-0) katika ligi ya kwao, yeye akifunga mabao yote manne.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu hii wa www.azamfc.co.tz Tchetche alisema ana furaha kubwa kufunga mabao hayo huku akidai kuwa amekuwa akijitahidi sana kila mara kujituma na kufanya vema uwanjani.

“Sina cha kusema sana, ila ni muendelezo wa kujituma uwanjani kwa ajili ushindi na kupata matokeo mazuri kwenye mechi,” alisema.

Tchetche mpaka sasa kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ameshafunga mabao tisa akiwa ndiye mfungaji kinara wa Azam FC akifuatiwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Shomari Kapombe wenye mabao nane kila mmoja.

Anaizungumziaje Esperance?   

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB imekata tiketi ya kukutana na Esperance ya Tunisia kwenye raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Bidvest Wits kwa jumla ya mabao 7-3.

Akizungumzia kwa kifupi mtanange huo, Tchetche alisema: “Itakuwa ni mechi nzuri, kwani ni moja ya timu nzuri (Esperance), tunatakiwa kufanya kazi vizuri zaidi ya tulivyofanya kwenye raundi ya kwanza.”

Mchezaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/14, aliendelea kusema kuwa Azam FC inayo nafasi ya kusonga mbele dhidi ya Esperance kwani watapambana wote uwanjani kila upande ukiwa na wachezaji 11  katika mechi hizo mbili za nyumbani na ugenini.

Mechi ya kwanza kati ya timu hizo itafanyika ndani ya Uwanja wa Azam Complex Aprili 10 mwaka huu huku wa marudiano ukipigwa wiki moja baadaye na mshindi wa jumla atafuzu kwa hatua ya mwisho ya mtoano kwa kucheza na timu iliyotoka katika Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kuingia hatua ya makundi (robo fainali).