KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa wanafuraha kukutana na Esperance ya Tunisia moja ya timu kubwa barani Afrika, kwenye raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, imepata nafasi hiyo baada ya kuitoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 7-3 huku Esperance nayo ikiitoa Renaissance ya Chad kwa ushindi wa jmla wa mabao 7-0.

Mabingwa hao wa Kombe la Kagame, wataanza kuikaribisha Esperance ndani ya Uwanja wa Azam Complex Aprili 10 mwaka huu kabla ya kurudiana nayo ugenini jijini Tunis wiki moja baadaye na mshindi wa jumla atavuka katika hatua ya mwisho ya mtoano kabla ya kuingia hatua ya makundi (robo fainali).

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu hii wa www.azamfc.co.tz Hall alisema watafanya maandalizi mazuri pamoja na kazi nzuri huku akijinasibu kuwa kuna malengo wamejiwekea.

“Tuna furaha kukutana na Esperance ni moja ya timu kubwa barani Afrika, hivyo tunataka kucheza na Esperance, unajua ni jambo zuri, ni jambo zuri kwa klabu, jambo zuri kwa wachezaji wetu na kila mtu anafuraha,” alisema.

Hii ni mara ya pili kwa Azam FC kufika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ikiwa chini Hall mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 2013, ilipotolewa na FAR Rabat ya Morocco kwa jumla ya mabao 2-1, ilitoka suluhu nyumbani kabla ya kufungwa 2-1 jijini Rabat huku nahodha John Bocco ‘Adebayor’ akikosa penalti dakika za mwisho ambayo ingeivusha timu hiyo.

Alichoongea vs Bidvest Wits?

Akizungumzia mchezo uliopita dhidi ya Bidvest, Hall alisema walishindwa kucheza vizuri kipindi cha kwanza hasa baada ya wapinzani wao kubadilisha mfumo kwa kutumia washambuliaji watatu.

“Kipindi cha pili tulikuwa na matatizo, walibadilisha mfumo walitumia washambuliaji watatu dhidi ya mabeki wetu watatu wa kati na hatukuweza kufanyia kazi mabadiliko hayo ipasavyo, nimefurahishwa na matokeo tuliyopata lakini kimbinu tulifanya baadhi ya vitu vibaya.

“Mabeki wetu wa pembeni ambao pia hushambulia kama winga (wingbacks) walikuwa mbali sana kutoa msaada pale washambuliaji watatu wa Bidvest walipokuwa wakikabiliana na mabeki wetu wa kati, hao walitakiwa kuingia ndani na kuwasaidia mabeki hao lakini walishindwa kufanya hivyo,” alisema.

Alimalizia kwa kusema kuwa ilikuwa ni rahisi sana kwa Bidvest kuwashambulia kipindi cha pili kutokana na udhaifu huo.