KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, ipo kamili kabisa kuikabili Bidvest Wits ya Afrika Kusini katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex kesho saa 9.00 Alasiri.

Kikosi cha Azam FC kinaingia na morali kubwa kwenye mchezo huo baada ya awali kutoka kushinda ugenini mabao 3-0 uliofanyika jijini Johannesburg wikiendi iliyopita huku Jumatano iliyopita ikiichapa Stand United bao 1-0.

Mashujaa wa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB kwenye mchezo huo wa kwanza walikuwa ni nahodha John Bocco ‘Adebayor’, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na beki Shomari Kapombe waliofunga mabao hayo pekee.

Hivyo Azam FC inahitaji ushindi au sare yoyote au isifungwe zaidi ya mabao mawili bila majibu ili kuweza kusonga mbele kwa raundi ya pili itakayofanyika mwezi ujao, ambapo kuna uwezekano ikakutana na Esperance ya Tunisia ambayo imeifunga Renaissance ya Chad mabao 2-0 na leo wanatarajia kurudiana jijini Tunis.

Alichosema Stewart Hall

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, leo ameuambia mtandao rasmi wa klabu hii wa www.azamfc.co.tz kuwa alicholenga kwenye mchezo huo ni ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele kwa raundi ya pili.

“Tunaingia kwenye mchezo huo kusaka ushindi, tunajua wenzetu wametuma kikosi mchanganyiko wa vijana na wazoefu, hivyo tumejipanga kupata ushindi dhidi yao,” alisema.

Hall alisema ataingia na kikosi kilichopata ushindi kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika wikiendi iliyopita na kuwapumzisha baadhi waliofanya kazi kubwa katika mechi ya ligi dhidi ya Stand United.

“Kuna baadhi ya wachezaji walicheza Afrika Kusini, lakini nikawapumzisha dhidi ya Stand United hivyo watarejea kwenye mchezo huo wakiwa fiti kabisa, Sure Boy (Salum Abubakar) yupo fiti pamoja na Michael (Bolou) na Himid (Mao) ambao walicheza vizuri katika eneo la kiungo dhidi yao, Messi (Ramadhan Singano), John Bocco na Kipre Tchetche nao wako fiti.

“Unapocheza katika joto kali, jambo kubwa la kuzigatiwa ni lazima wachezaji wote unaowatumia lazima wawe kwenye kiwango kimoja cha nguvu, mchezaji hupoteza nguvu nyingi sana katika hali ya hewa hiyo, na ndio maana tunafanya mabadiliko kila mara, utakuta leo Domayo (Frank) anacheza na kesho atapumzika na kucheza Migi (Jean Mugiraneza),” alisema.

Mwingereza huyo alimalizia kwa kusema kuwa kwa sasa haifikirii Esperance  ambayo ina nafasi kubwa ya kukutana nao kwenye raundi ya pili akidai kuwa atapomalizia kazi ya kuitoa Bidvest ndio ataanza kuiwazia timu hiyo.

Viingilio vya mchezo huo

Kuhusiana na tiketi za mchezo huo, zitaanza kuuzwa kesho asubuhi kwenye vituo viwili vya Dar Live (Mbagala) na nje ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Makundi ya tiketi hizo, kiingilio cha chini kabisa kitakuwa ni Sh. 3,000 kwa majukwaa ya mzunguko huku V.I.P A kikiwa ni Sh. 15,000 na V.I.P B Sh. 10,000.

Rekodi ya Azam FC CAF nouma

Azam FC imekuwa na rekodi nzuri ya kutumia vema uwanja wa nyumbani kwenye michuano ya CAF kwani haijawahi kufungwa mchezo wowote kwenye mechi tano ilizocheza jijini Dar es Dar es Salaam ikishinda tatu na sare mbili.

Mwaka 2013 ilitumia Uwanja wa Taifa kama uwanja wa nyumbani na kuzifunga Al Nasri ya Juba, Sudan Kusini (3-1) a kusonga mbele kwa jumla ya mabao 8-1, raundi ya kwanza ikatoa suluhu dhidi ya Barrack Young Controller nyumbani kabla ya kuitandika 2-1 ugenini, kisha raundi ya pili ikatoa suluhu tena nyumbani walipocheza FAR Rabat ya Morocco na kufungwa 2-1 ugenini.

Mwaka juzi Azam FC ikatumia Uwanja wa Azam Complex wakati ikishiriki tena Kombe la Shirikisho Afrika na kuichapa Ferroviario da Beira 1-0 nyumbani kabla ya kutolewa ugenini kwa kufungwa 2-0.

Mwaka jana ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) 2013/14, bila kufungwa mchezo wowote, ambapo iliwafunga waarabu hao 2-0 nyumbani kabla ya kutolewa ugenini kwa kuruhusu mabao 3-0 na mwaka huu inashiriki michuano ya CAF kwa mara ya nne mfululizo.