KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imezidi kufanya kweli kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya jioni ya leo kuichapa Stand United bao 1-0 katika mchezo mkali uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Alikuwa ni beki wa kulia Shomari Kapombe, aliyeihakikishia pointi tatu muhimu Azam FC baada ya kufunga bao zuri dakika ya 62 akiserereka chini na kupiga shuti lililigonga nyavu za juu akimalizia krosi safi ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Allan Wanga.

Wikiendi iliyopita Kapombe alifunga moja ya mabao ya Azam FC wakati ikiilaza ugenini Bidvest Wits ya Afrika Kusini, mengine yakifungwa na Bocco na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Katika mchezo wa leo Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, aliwapumzisha baadhi ya nyota wa kikosi cha kwanza ili kuwa fiti kuelekea mchezo wa Jumapili ijayo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bidvest Wits.

Azam FC iliuanza vema mchezo huo na iliwachukua sekunde ya 20 tu kulifikia lango la Stand United kwa kufanya shambulizi kali lakini shuti lililopigwa na Kipre Tchetche akiwa ndani ya eneo la 18 lilipita pembeni ya lango.

Tchetche alijaribu tena kuipa bao la uongozi Azam FC dakika ya pili baada ya kuwapiga chenga walinzi wawili wa Stand United lakini shuti alilopiga lilitoka nje kidogo ya lango.

Stand United kucheza kwa kulundikana eneo moja kila Azam FC ilipokuwa na mpira kuliwanyima mabingwa hao nafasi ya kuuchezea mpira hasa safu ya ushambuliaji iliyokuwa ikiundwa na Tchetche aliyekuwa akisaidiana na Wanga na hivyo kufanya kipindi cha kwanza kuisha kwa suluhu.

Mabingwa hao wa Kombe la Kagame wanaodhaminiwa na Benki bora kabisa nchini Tanzania ya NMB iliyosambaa kwenye mikoa yote nchini, walianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko akitoka Wanga na nafasi yake kuchukuliwa na Bocco.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Azam FC hasa baada ya Bocco kuanza kuisumbua na kuipa wakati mgumu ngome ya ulinzi, akicheza kwa kuzunguka kila upande ndani ya eneo la ushambuliaji.

Hatimaye shambulizi alilolifanya dakika ya 62  lilizaa matunda ya kupatikana bao hilo pekee la Azam FC likisukumwa wavuni na Kapombe, ambaye amefikisha bao la 10 msimu huu kwenye mashindano yote na bao la nane Ligi Kuu.

Hadi dakika 90 za mwamuzi Ngole Mwangole kutoka mkoani Mbeya zinamalizika, walikuwa ni Azam FC walioweza kuibuka kifua mbele na kuzoa pointi zote tatu.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kuifikia Yanga kwa pointi, wote wakiwa nazo 50 huku akiwa ameachwa kwa pointi nne na kinara Simba iliyojikusanyia jumla ya pointi 54 lakini iko mbele kwa michezo miwili dhidi ya wapinzani wake hao katika mbio za ubingwa.

Kikosi cha Azam FC kiliundwa;    

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Farid Mussa/Wazir Salum (dk 65), Aggrey Morris, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Jean Mugiraneza, Frank Domayo, Mudarhir Yahya/Michael Bolou (dk 79), Kipre Tchetche, Allan Wanga/John Bocco (C) dk 45.