TIMU ya vijana ya Azam FC ‘Azam FC Academy’ mchana wa leo imewashushia kipigo kizito vijana wenzao wa Ramonda baada ya kuichapa mabao 7-1, mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex.

Mchezo huo ulikuwa ni mahususi kwa kuikaribisha mechi ya wakubwa ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kati ya wenyeji Azam FC na Stand United itakayofanyika jioni ya leo.

Azam Academy iliuanza vema mchezo huo na kupata bao la mapema lililofungwa dakika ya tatu na mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Shabaan Idd kabla ya Yahaya Zaidi kuongeza la pili dakika tatu baadaye.

Juhudi za kusaka mabao zaidi zilizaa matunda tena dakika ya 12 baada ya Shaaban kuifungia Azam FC Academy bao la tatu huku Optatus Lupekenya akishindilia msumari wa mwisho wa nne wa timu hiyo kwa kipindi cha kwanza.

Ramonda nao hawakuwa nyuma kwani walifanikiwa kujipatia bao la kufuatia machozi lililofungwa dakika ya 36 na Hillary Humud.

Kipindi cha pili Azam FC Academy inayonolewa na Mwingereza Tom Legg na Msaidizi wake Idd Cheche, iliendeleza kasi yake iliyoanza nayo kipindi cha kwanza hasa sehemu ya kiungo iliyokuwa ikiundwa na nahodha Masoud Abdallah ‘Cabaye’, Yahaya na Rajab Odasi ikionekana kutakata.

Mabao mengine ya Azam FC Academy yalifungwa na washambuliaji waioingia kipindi cha pili Yohana Mkomola, aliyechukua nafasi ya Shaaban na Mohamed Sadallah aliyeingia badala ya  Optatus. Mkomola aliyeingia na kasi kubwa alitupia la bao la tano dakika ya 61 kabla ya Sadallah kuongeza mwengine mawili dakika ya 66 na 68 na kufanya mchezo huo kuisha kwa ushindi huo mnono wa Azam FC Academy ambayo jana asubuhi iliichapa Villa Squad mabao 2-1.

Katika mchezo huo ilishuhudiwa beki wa timu ya wakubwa Abdallah Kheri Sebo akicheza kipindi cha kwanza ili kutafuta ufiti baada ya kutoka kwenye majeraha ya enka aliyopata mazoezini wakati Azam FC ikijiandaa na mchezo dhidi ya Coastal Union.