KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kesho saa 10.30 jioni itaendeleza kampeni ya kuwania taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuikaribisha Stand United ya Shinyanga katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya wikiendi iliyopita kuilaza Bidvest Wits mabao 3-0, mechi iliyofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Kuelekea mchezo huo, Azam FC inayodhaminiwa na Benki bora kabisa nchini Tanzania ya NMB imekuwa ikifanya mazoezi ya nguvu ya kuwakabili vema Stand United tokea jana mara baada ya kurejea kutoka nchini Afrika Kusini Jumapili iliyopita jioni.

Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu Stewart Hall na Wasaidizi wake, Mario Marinica na Dennis Kitambi, limepanga kuwapumzisha baadhi ya nyota waliofanya kazi kubwa nchini Afrika Kusini na kuwatumia wale waliokuwa fiti asilimia 100 ili kuonyesha kiwango kizuri dhidi ya Stand United.

Ikumbukwe kuwa siku nne baadaye mara baada ya mtanange huo Azam FC itashuka tena dimbani kucheza mchezo muhimu wa marudiano dhidi Bidvest Wits utakaofanyika Jumapili ijayo (Machi 20) saa 9.00 Alasiri ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

Rekodi zao mpaka sasa?

Mpaka sasa kihistoria timu hizo zimekutana mara tatu tokea Stand United ipande Ligi Kuu msimu uliopita, mara zote hizo Azam FC imeibuka kidedea kwa kupata ushindi mechi zote huku ikiwa haijafungwa bao hata moja na Stand United.

Katika mechi zote hizo tatu, Azam FC imefunga jumla ya mabao saba huku ushindi mnono walioupata ukiwa ni wa mabao 4-0 walioupata Azam Complex Aprili 25 mwaka jana, yaliyofungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo Brian Majwega, Gaudence Mwaikimba aliyetupia mawili pamoja na kinda Farid Mussa.

Azam FC iliitambia Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa kuichapa mabao 2-0, yaliyosukumizwa wavuni na Mkenya Allan Wanga na kiungo fundi Frank Domayo aliyepiga shuti kali katikati ya uwanja, moja ya bao ambalo ni bora kabisa mpaka sasa kwenye ligi hiyo.

Msimamo wao msimu huu?

Mabingwa hao wa Ligi Kuu msimu wa 2013/14 bila kupoteza mchezo wowote, mpaka sasa imefanikiwa kucheza jumla ya mechi 20, ikishinda 14, sare tano na kufungwa mmoja wakiwa katika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia jumla ya pointi 47.

Lakini inazidiwa mchezo mmoja na anayeshika nafasi ya pili Yanga waliojikusanyia pointi 50 na pia ina michezo mitatu mkononi dhidi ya Simba iliyoko kileleni waliojikusanyia pointi 54.

Hivyo ushindi wowote kesho utaifanya kufikia pointi za Yanga na kuendeleza kasi ya kuwania taji la ligi hiyo, ambayo imebakisha takribani mechi saba na nyingine 10 ili kuweza kuitimika na bingwa kujulikana.

Stand United yenyewe haijapata ushindi ndani ya mechi sita zilizopita za ligi, kati ya hizo imefungwa nne na kuambulia sare mbili, ambapo mara ya mwisho ilishinda dhidi ya Toto Africans mabao 2-1 Januari 20 mwaka huu.

Timu hiyo ya Shinyanga mpaka sasa imejikusanyia jumla ya pointi 30 katika nafasi ya saba ikishinda mara tisa, sare tatu na kufungwa mechi 10.

Nyota wanaozing’arisha?

Nyota watatu wa Azam FC, Kipre Tchetche, nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Shomari Kapombe, wao ndio vinara wa walioifungia timu hiyo mabao mengi msimu huu wa ligi hiyo.

Tchetche ndio anayeongoza akiwa na mabao tisa, Bocco akifunga nane na Kapombe aliyekuwa kwenye kiwango bora kabisa akiwa ametupia nyavuni mabao saba kuliko beki mwingine yoyote katika ligi hiyo.

Stand United imekuwa ikimtegemea zaidi mshambuliaji Elias Maguli aliyepachika mabao 10 mpaka sasa, ambaye amepungua makali yake baada ya kuanza mzunguko wa pili wa ligi kutokaa na kuwekwa benchi kwenye mechi nyingi za timu hiyo chini ya Kocha Mfaransa Patrick Liewig.