BEKI kisiki wa kati wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aggrey Morris, amerejea uwanjani na ari mpya ya kufanya makubwa huku akitamba kuwa amekuja na nguvu mpya ya kuisaidia timu hiyo.

Morris aliyerejea uwanjani kwa mara ya kwanza wikiendi iliyopita Azam FC ilipoichapa Bidvest Wits mabao 3-0, alikosekana dimbani kwa takribani miezi mitatu akiuguza majeraha ya goti aliyopata akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Zanzibar.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu hii wa www.azamfc.co.tz mara baada ya kurejea dimbani, Morris alisema alikuwa akiumia sana alipokuwa nje ya dimba kutokana na kutamani mno kuisaidia Azam FC.

“Nafurahi sana kurejea dimbani tena, nilikuwa natamani sana kucheza, kuna muda nilikuwa naumia sana nilipokuwa naona timu yangu inahitaji msaada wangu na mimi pia nilikuwa natamani kuisaidia, sisi wachezaji tunapenda kucheza, nilihisi kuna kitu naweza kuisaidia timu yangu kwa hiyo nafurahia kurejea na najua nitatoa mchango kwa timu yangu,” alisema.

Beki huyo mwenye uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya juu na chini anayecheza kwenye kikosi kinachodhaminiwa na Benki ya NMB, alichukua fursa hiyo kuwaomba mashabiki wa Azam FC wazidi kuwa pamoja naye huku akiwaahidi kujitolea kwa uwezo wake wote kuwasaidia mabingwa hao.

“Mimi nawaambia mashabiki waendelee kuwa nami, kwa sababu najua walimiss kwa kipindi kirefu na wamenivumilia kusema kweli na wamenisapoti kwa kipindi chote kigumu pia watarajie tu kujitoa kwa moyo wangu wote kuisaidia timu yangu,” alimalizia Morris.