KIUNGO wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, amekuwa gumzo nchini Afrika Kusini baada ya kuonyesha kiwango kizuri wakati timu hiyo ilipomenyana na Bidvest Wits ya huko kwenye Uwanja wa Bidvest Jumamosi iliyopita.

Azam FC ilishinda mabao 3-0 kwenye mchezo huo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika na sasa zitarudiana Jumapili hii (Machi 20) katika Uwanja wa Azam Complex.

Sure Boy ndiye aliyefunga bao la ufunguzi la Azam FC kwa shuti kali la chini lililombabatiza mlinzi mmoja wa Bidvest na kujaa wavuni, mengine yakifungwa na Shomari Kapombe na nahodha John Bocco ‘Adebayor’.

Kabla ya kufunga bao hilo kiungo huyo alifanikiwa kupiga mashuti mengine matatu nje ya eneo la 18, ambayo yalipaa juu ya lango la Wits lakini shuti la nne lilijaa wavuni baada ya kuufumania mpira nje ya eneo la 18 kufuatia kona safi iliyochongwa na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Ubora wa Sure Boy kwenye mchezo huo ulitokana na ushirikiano mzuri waliotengeneza na viungo wenzake nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’ na Michael Bolou, ambao walikuwa na majukumu ya kukaba na hivyo kuwadhibiti vilivyo viungo wa Bidvest Wits.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika wakazi wengi wa Afrika Kusini walioshuhudia mchezo huo na hata baadhi ya makocha wa Wits walionekana kuridhishwa na uwezo wa Sure Boy wakitaja jezi yake namba nane aliyokuwa amevalia.

Mbali na ubora wa Sure Boy kwenye mchezo huo, Azam FC ilifanikiwa kucheza vema katika maeneo yote ya uwanja kuanzia eneo la ulinzi hadi ushambuliaji, hali iliyowafanya Wits kuwa na wakati mgumu zaidi kwa dakika zote 90 za mtanange huo.

Azam FC inahitaji ushindi wowote au sare kwenye mchezo huo wa marudiano na isiruhusu zaidi ya mabao mawili ili kusonga mbele huku Wits ikiwa na mlima mrefu wakitakiwa kuipiga mabao 4-0 mabingwa hao ili kupenya kwa raundi ya pili.

Mshindi yoyote wa jumla wa mchezo huo atasonga mbele kwa raundi ya pili ambapo atakutana na moja ya timu kati ya Esperance ya Tunisia au Renaissance ya Chad, ambayo imefungwa mabao 2-0 na waarabu hao kwenye mechi ya kwanza wakiwa nyumbani jijini N’Djamena.