KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, ipo kamili kabisa kuingia vitani na kusaka matokeo bora katika mchezo huo muhimu wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bidvest Wits utakaofanyika kesho saa 1.00 usiku katika Uwanja wa Bidvest.

Huo ni mchezo wa kwanza kwa Azam FC kwenye michuano ya kimataifa iliyosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwaka huu, mara baada ya mechi hiyo watarudiana na timu hiyo wiki moja ijayo (Machi 20) kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Kuelekea mchezo huo yafuatayo ni mambo muhimu kuhusu timu zote mbili na namna Azam FC ilivyojipanga vema kusaka ushindi wa ugenini dhidi ya Bidvest Wits inayojiita jina la utani la Clever Boys.

Changamoto za uwanjani?

Benchi la ufundi la Azam FC chini ya Mwingereza Stewart Hall na Wasaidizi wake, Mario Marinica na Dennis Kitambi, mpaka sasa limefanya kazi kubwa ya kuwasoma wapinzani wao na limekuwa likifanya vikao na wachezaji mara kwa mara ili kuwapa mbinu za kukabiliana na Bidvest kwa kujua udhaifu na upungufu wao.

Hivyo pamoja na ugumu wa mchezo huo wa ugenini, tayari wachezaji wa Azam FC wanajua namna gani ya kukabiliana na wapinzani wao kutokana na mafunzo wanayopewa nje ya uwanja kupitia DVD za mechi zao na ndani ya uwanja kwa kupewa mbinu sahihi za kushinda vita hiyo.

Akizungumzia suala hilo, Hall amesema wamewasoma wapinzani wao kupitia DVD na mchezo mmoja ‘live’ na wamebaini kuwa wapinzani wao wamefunga mabao mengi kupitia mipira ya krosi, kona na adhabu ndogo.

“Pia tumeangalia wachezaji wao mmoja mmoja na kujua bora, wote tunao wasifu wao na pia aina ya uchezaji wao, kama nilivyosema wanatumia mipira mirefu na kufunga kupitia mipira ya krosi, kona na adhabu ndogo, yote hayo tumeyafanyia kazi.

“Hatutacheza kwa kuwazuia wao tu, kwani huwezi kucheza hivyo na kusahau wewe unatakiwa kucheza vipi, namna gani utakavyocheza wewe ndio jambo la muhimu na namna utakavyowazuia inatakiwa kuendana na staili ya uchezaji wako,” alisema Hall.

Hali ya hewa?

Azam FC tokea iwasili jijini Johannesburg imekutana na hali ya hewa ya baridi kiasi na mvua zinazonyesha, hivyo kikosi hicho kimejipanga vilivyo kukabiliana na hali ya hewa hiyo na kupata matokeo.

Kama hiyo haitoshi timu hiyo imenunua viatu maalumu vya kukabiliana na Uwanja wa Bidvest pamoja na mvua kama itanyesha, yote hayo yamefanyika ili kuwaweka wachezaji katika mazingira mazuri ya kupata matokeo mazuri.

Jambo kubwa na la kupendeza hali ya hewa ya hapa inafanana sana na ile waliyokutana nayo nchini Zambia walipokwenda kushiriki michuano maalumu ya timu nne (Zesco United, Zanaco FC na Chicken Inn) na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, hivyo kambi hiyo ya jijini Ndola imeanza kuipa faida Azam FC.

“Tumejiandaa kupambana na hali ya hewa ya hapa kwa sababu ni tofauti sana, pia nyasi za uwanja tutakaotumia zimenyooka na ni za kijani na unaruhusu soka kuchezwa kwa haraka sana, vilevile hali ya hewa ni mvua, na katika kujipanga na mazingira yote hayo kila mchezaji anacho kiatu cha kukabiliana na hayo,” alisema Hall.   

Rekodi ya Kocha Stewart Hall?

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Kocha Mkuu Stewart Hall, kuiongoza Azam FC kwenye michuano hiyo, kwa mara ya kwanza aliweza kuifikisha katika hatua ya 16 bora rekodi ambayo imeshindwa kufikiwa na kocha aliyekuja nyuma yake kwa miaka miwili iliyopita.

Hall hadi anafika hatua hiyo alifanikiwa kuitoa timu ya El Nasir ya Juba kwa jumla ya mabao 8-1 raundi ya awali, ikaitupa tena nje Barrack Young Controllers II ya Liberia kwa ushindi wa 2-1 kabla ya kutolewa na FAR Rabat ya Morocco (2-1).

Katika mchezo huo dhidi ya Wamorocco, Azam FC ingeweza kusonga mbele kama nahodha wake John Bocco ‘Adebayor’ angefunga penalti waliyoipata dakika za mwisho ambayo ingefanya matokeo kuwa 2-2 na kuvuka kwa faida ya mabao ya ugenini lakini aliikosa.

Hall amesema amepanga kuikifikisha mbele zaidi Azam FC kuizidi rekodi hiyo aliyoiacha na ana malengo makubwa aliyowekewa na Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo ni kufika hatua ya makundi (robo fainali) ya michuano hiyo mwaka huu.

Wachezaji watakaokosekana?

Kocha huyo wa zamani wa Zanzibar Heroes na Sofapaka ya Kenya, alimalizia kwa kusema kuwa wachezaji wote wapo fiti kuelekea mchezo huo isipokuwa mabeki wawili Abdallah Kheri Sebo na Racine Diouf, ambao wamebakishwa jijini Dar es Salaam kutokana na kuwa majeruhi pamoja na beki Aggrey Morris aliyeko huku jijini Johannesburg ambaye bado hajawa fiti asilimia baada ya kutoka kuuguza majeraha ya goti.