NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amesema kuwa wana morali kubwa kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini keshokutwa Jumamosi na kuwaahidi Watanzania kuwa watapambana uwanjani ili kuwapa matokeo mazuri.

Mchezo huo wa raundi ya kwanza utafanyika katika Uwanja wa Bidvest uliopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini kuanzia saa 1.00 kwa saa za Afrika Mashariki huku ule wa marudiano ukitarajia kupigwa Machi 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam kuanzia saa 9.00 Alasiri.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu hii www.azamfc.co.tz Bocco alisema wanajua kuwa wapinzani wao ni timu nzuri lakini wamejopanga kujituma kwa dakika zote tisini uwanjani kutimiza malengo waliyojiwekea ili kusonga mbele.

“Tumejiandaa vizuri kwanza tunamshukuru Mungu kwa kufika salama, tumefanya mazoezi yetu ya kwanza jana tumekutana na hali ya hewa tofauti na nyumbani, kuna hali ya hewa ya mvua na baridi lakini naamini haiwezi ikatushida sisi kutimiza malengo yetu yaliyotuleta huku,” alisema.

Bocco ambaye pia nahodha msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, alizidi kuwaambia Watanzania kuwa: “Ninachowaahidi Watanzania na mashabiki wetu wa Azam FC kuwa watuamini, sisi kama timu iliyotoka Tanzania ni moja ya wawakilishi katika mashindani ya kimataifa, tumejipanga vizuri, tumejiandaa vizuri, wachezaji wana morali nzuri wana malengo yaliyokuwepo sawa wote ya kuweza kufanikiwa katika mchezo huo na mwingine unaokuja ili tuweze kufika raundi ya pili.”

Nyota huyo wa muda wote wa Azam FC pia alizungumzia rekodi mbaya ya kutofanya vizuri katika michuano ya kimataifa kwa misimu miwili iliyopita kwa kusema kuwa: “Ni kweli kwa misimu miwili iliyopita tumepata nafasi ya kushiriki kwenye mashindano haya lakini tuliweza kutoka katika raundi ya kwanza, naamini kama klabu tumejifunza wapi tulipoteleza na wapi tunatakiwa kuboresha ili msimu huu tuweze kufika mbele.

“Naamini na baadhi ya wachezaji wengi walikuwepo katika misimu hiyo miwili pia wapo hadi sasa hivi kuna baadhi ya vitu wamejifunza na naamini maandalizi ya msimu huu pia yamekuwa ni mazuri zaidi kuliko hata misimu iliyopita kwa hiyo nina imani kubwa msimu huu tutafika mbali zaidi,” alisema

Kikosi cha Azam FC tokea kiwasili jana mchana jijini Johannesburg kimefikia katika Hoteli ya kifahari ya Garden Court na jioni yake ilifanya mazoezi kwenye mvua saa 12.50 kwa saa za Afrika Mashariki hasa kutokana na hali ya hewa ya mvua inayoendelea huku na leo saa 11 jioni itafanya mengine ndani ya Uwanja wa timu ya Chuo cha Wits.

Hii itakuwa ni mara ya nne mfululizo kwa Azam FC kushiriki michuano hiyo ya kimataifa ya CAF na bahati iliyoje msimu huu imekuwa timu pekee ya Afrika Mashariki kuanzia raundi ya kwanza kwani nyingine zimeanzia raundi ya awali.