SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limewaweka wazi waamuzi watakaochezesha mechi mbili za raundi ya kwanza  ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Azam FC na Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

Mchezo wa kwanza wa raundi hiyo utafanyika kwenye Uwanja wa Bidvest jijini Johannesburg, Afrika Kusini Jumamosi hii (Machi 12) kuanzia saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, ambapo unatarajia kuchezeshwa na waamuzi kutoka nchini Madagascar.

Mwamuzi wa kati anatarajia kuwa Andofetra Avombitana Rakotojaona, akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Pierre Jean Eric Andrivoavonjy huku msaidizi namba mbili akiwa Lionel Hasinjarasoa Andrianantenaina.

Wakati waamuzi hao wakiamua mtanange huo wa kwanza, dakika 90 zingine za mchezo wa marudiano utakaofanyika ndani ya Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam Machi 20 mwaka huu saa 9.00 Alasiri zinatarajia kuamuliwa na waamuzi kutoka nchini Sudan Kusini.

Mwamuzi wa kati atakuwa Gait Metodious Oting, Msaidizi namba moja anatarajia kuwa Abdalla Suleiman Gassim pamoja na Gasim Madir Dehiya, atakayekuwa msaidizi namba mbili.

Kuelekea mchezo huo kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka leo saa 4 asubuhi kwa Shirika la Ndege ya FastJet kwenda jijini Johannesburg kwa ajili ya kuivaa Bidvest ambao jina lao la utani ni ‘Clever Boys’.