NYOTA saba wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, wameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kitakachojiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Chad, utakaofanyika Machi 23 mwaka huu jijini N’Djamena.

Wachezaji wa Azam FC walioitwa ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe huku Erasto Nyoni na David Mwantika wakirejeshwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho chini ya Kocha Mkuu Charles Boniface Mkwassa.

Viungo ni Himid Mao ‘Ninja’ na winga Farid Mussa pamoja na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’, ambaye ni nahodha wa Azam FC na nahodha msaidizi wa Stars.

Wachezaji wa timu nyingine waliojumuishwa ni makipa Ally Mustapha ‘Barthez’ (Yanga) na Shaban Kado (Mwadui), mabeki Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani (Yanga) na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba).

Mkwassa pia amewajumuisha viungo Ismail Juma (JKU), Jonas Mkude, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto (Simba), Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar) na Deus Kaseke (Yanga).

Washambuliaji ni nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Elias Maguri (Stand United), Jeremia Mgunda (Tanzania Prisons) na Ibrahim Ajibu (Simba).