KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imewaahidi Watanzania kuwa watawafanya watembee kifua mbele na kujivuna kwa kuwapa matokeo mazuri watakapocheza na Bidvest Wits ya Afrika Kusini Jumamosi ijayo (Machi 12) kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC itaanza kuchanga karata yake ya kwanza kwenye michuano hiyo kwa kucheza ugenini jijini Johannesburg dhidi ya Bidvest kuanzia saa 1.00 jioni kwa saa Afrika Mashariki, mchezo utakaofanyika ndani ya Uwanja wa Bidvest.

Wakati Azam FC ikianzia raundi hiyo ya kwanza, Bidvest Wits imefika hatua hiyo baada ya kuiondosha Light Stars ya Seychelles kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-0, ikianza kwa kushinda ugenini 3-0 kabla ya kuichapa tena 6-0 nyumbani.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz Kocha Msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica, alisema wameiona Bidvest Wits kwenye mechi kadhaa na wanajua mbinu wanazotumia na kudai kuwa wanayo nafasi nzuri ya kuwatoa Wasauzi hao.

“Tunauchukulia mchezo huo kwa uzito mkubwa, hata wapinzani wetu nao tunawachukulia kwa uzito mkubwa, tayari tumeshawapeleleza kwenye mechi kadhaa, tunajua ubora wao na ni timu nzuri, ila sisi tuko kamili na tayari kucheza nao,” alisema.

Marinica aliyekwenda kuipeleleza Bidvest Wits wakati ikiichapa Light Stars ya Seychelles mabao 3-0  kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo, akiwa sambamba na Kocha mwingine Msaidizi Dennis Kitambi, alisema kuwa Azam FC ina nafasi kubwa ya kusonga mbele dhidi ya Wasauzi hao kutokana na ubora wa kikosi walichonacho.

“Sisi tuna kikosi bora, lakini tatizo kubwa tulilonalo kikosini ni kushindwa kutumia vema nafasi tunazotengeneza za kufunga mabao, vinginevyo mimi nadhani na kujiamini kuwa tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri dhidi ya Bidvest kama tukicheza kwa staili yetu tunayocheza hivi sasa,” alisema.

Kocha huyo raia wa Romania alikumbushia ubingwa wa michuano ya Kagame waliotwaa Agosti mwaka jana kwa kusema kuwa: “Tulicheza dhidi ya mabingwa wa nchi 11 kwenye Kombe la Kagame na tukachukua ubingwa bila kufungwa mchezo wowote wala kuruhusu bao, naamini ya kuwa tutamfurahisha kila Mtanzania dhidi Bidvest kwa kupata matokeo mazuri.”

Mara baada ya mchezo huo wa kwanza, Azam FC itarudiana na Bidvest baada ya wiki moja ndani ya Uwanja wa Azam Complex Machi 20 mwaka huu, itakayoanza kutimua vumbi kuanzia saa 9.00 Alasiri na mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa jumla kati ya timu ya Renaissance ya Chad na Esperance de Tunis ya Tunisia kwenye raundi ya pili itakayoanza kutimua vumbi Aprili mwaka huu.