TIMU ya vijana ya Azam FC ‘Azam FC Academy’ jana iliwafunza soka vijana wenzao wa Yanga baada ya kuichapa mabao 2-1.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam saa 7.00 mchana kabla ya ule wa wakubwa zao, ulikuwa mkali na wa aina yake kutokana na ufundi uliokuwa ukonyeshwa na wachezaji wa pande zote mbili.

Bao la uongozi la Azam FC Academy limefungwa na mshambuliaji wa timu hiyo, Mohamed Sadallah kipindi cha kwanza kabla ya Yanga kusawazisha bao hilo kupitia mkwaju wa penalti.

Wakati watu wakidhania mtanange huo ungeisha kwa sare, Azam FC iliweza kujipatia bao safi la pili lililofungwa na mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Shaaban Idd kwa shuti kali nje ya eneo la 18 baada ya kuwahadaa mabeki wa Yanga na kupiga shuti kali lililojaa wavuni.

Mashabiki wengi waliokuwa wakishuhudia mchezo huo walionekana kulifurahia bao hilo kwa kulishangilia hasa kutokana na mfungaji kutumia akili za ziada hadi anafunga.

Huo ni mwendelezo mzuri wa kikosi hicho kinachonolewa na Mwingereza Tom Legg na Msaidizi wake Idd Cheche, ambacho kimeendelea kuvuna ushindi kila kukicha sio kwa vijana wenzao tu bali hata kwa timu zinazoshiriki madaraja ya juu katika soka la Tanzania.