KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jioni ya leo imefanikiwa kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB ingeweza kuondoka na ushindi kwenye mchezo huo, kama maamuzi ya waamuzi Kennedy Mapunda (katikati), Frank Komba (msaidizi namba moja) na Soud Lilla (msaidizi namba mbili) yangefuata sheria 17 za soka.

Hiyo inatokana na mwamuzi Frank Komba kulikataa bao la wazi la Azam FC lililofungwa kwa kichwa na Shomari Kapombe dakika ya 20, akidai kuwa beki huyo wa kulia alikuwa ameotea kabla ya kufunga jambo ambalo lilikuwa si sahihi.

Wakati Kapombe akifunga bao hilo, Azam FC ilikuwa iko mbele kwa bao moja lililofungwa na beki wa Yanga, Juma Abdul, aliyejifunga dakika ya 10 wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa shuti kali lililopigwa na Kipre Tchetche.

Kabla hata ya Azam FC kupata bao hilo, dakika ya kwanza tu ya mchezo mwamuzi Kennedy Mapunda, alifanya maamuzi ya kutatanisha baada ya kumpa kadi ya njano kiungo Himid Mao ‘Ninja’, akidai amejiangusha ndani ya eneo la 18 ilihali ya kuwa alifanyiwa madhambi ya makusudi ambayo kwa tafsiri ya sheria 17 za soka, mwamuzi alitakiwa aamuru penalti ipigwe kuelekea lango la Yanga.

Hayo ni baadhi tu ya madudu ya waamuzi kwenye mchezo wa leo, ambao umeathiriwa kwa kiasi kikubwa na maamuzi mabovu ya waamuzi kwa kupindisha sheria 17 za soka na kuifanya mechi hiyo kuwa na hadhi ya chini.

Yanga ilirejea mchezoni dakika ya 28 baada ya kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Juma Abdul kwa shuti kali baada ya kukutana na mpira nje ya eneo la 18 uliotoka kuokolewa na beki wa Azam FC, Pacsal Wawa.

Yanga ilijipatia bao la pili dakika ya 41 lililofungwa na Donald Ngoma kwa kichwa akimalizia mpira wa kunyanyua uliopigwa na Amissi Tambwe na kufanya mpira kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza kwa mabao hayo.

Kipindi cha pili kilianza vema kwa upande wa Azam FC ambao walifanikiwa kukimiliki kwa kiasi kikubwa wakiongozwa na viungo Ramadhan Singano ‘Messi’, Himid Mao na Jean Mugiraneza, ambao walionyesha viwango bora kabisa kwenye mchezo huo.

Hata walipoingia Didier Kavumbagu (dk 59), Frank Domayo (dk 68) na Mudathir Yahya (dk 85), bado Azam FC iliendelea kutawala mchezo huo na kufanya mashambulizi makali ya kushtukiza langoni mwa Yanga.

Juhudi za Azam FC kusaka bao la kusawazisha zilizaa matunda dakika ya 70 baada ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’ kufunga bao hilo muhimu kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Yanga, Ally Mustafa, akimalizia pande safi alilowekewa na Kipre Tchetche.

Yanga ilionekana kuelemewa sana kuelekea dakika za mwisho za mchezo huo, lakini hadi dakika 90 zinamalizika tim hizo ziligawana pointi moja moja kufuatia suluhu hiyo.

Suluhu hiyo inamaanisha kuwa timu hizo zinabakia kileleni mwa msimamo wa ligi zikiwa zina pointi 47 kila mmoja, lakini Yanga yupo kileleni kwa uwiano mzuri wa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Ushindi wowote kwa Simba kesho dhidi ya Mbeya City utaifanya kupanda kileleni mwa msimamo, kwani watakuwa wamefikisha jumla ya pointi 48.

Kikosi Azam FC leo;

Aishi Manula, Shomari Kapombe, David Mwantika, Said Morad, Pascal Wawa, Farid Mussa/Didier Kavumbagu dk59, Jean Mugiraneza, Himid Mao/Frank Domayo dk68, Ramadhan Singano/Mudathir Yahya dk85, John Bocco na Kipre Tchetche.