KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mario Marinica, amesema kuwa hawana wasiwasi wowote na Yanga kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kesho (Machi 5).

Timu hizo mbili zinakutana wakati zikiwa na pointi sawa kwenye msimamo wa ligi, wote wakiwa na pointi 46 kileleni, lakini Yanga ipo juu kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa (GD), hivyo mchezo huo unatarajia kuwa na vita ya kuwania uongozi wa ligi na ile ya kuwania taji la ligi hiyo.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz Marinica alisema wanaijua vema Yanga na wamejipanga kucheza kiprofesheno kwa kutumia staili yao huku akiomba waamuzi wa mchezo huo kutenda haki.

“Tumecheza na Yanga mara nne msimu huu kwenye mashindano tofauti, licha ya waamuzi na TFF kuwa upande wao, hawajaweza kutufunga mchezo hata mmoja, uliona kilichotokea kwenye mchezo wetu wa mwisho Yanga alizawadiwa penalti ambayo haikuwa halali.

“Hata katika Kombe la Mapinduzi walipewa bao la kusawazisha ambalo halikuwa halali kwani mpira haukuvuka mstari, tena tulikuwa pungufu ya mtu mmoja baada ya Bocco kupewa kadi nyekundu, licha ya kila mbinu wanazotumia tukicheza nao bado wameshindwa kutufunga tena wakiwa nyumbani mechi zote, hii inaonyesha kuwa wao sio bora,” alisema.

Kocha huyo raia wa Romania alisema kuwa pambano hilo halitaamua bingwa wa ligi hiyo kwa atakayeshinda kama inavyodhaniwa na wengi kutokana na kubakia kwa mechi takribani kumi kwa kila timu baada ya mchezo huo.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki na NMB ilita sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, Kipre Tchetche aliyeingia kipindi cha pili akisawazisha bao lililofungwa na Donald Ngoma katika mechi ambayo mwamuzi Abdallah Kambuzi aliizawadia Yanga penalti dakika za mwisho iliyopigwa na kiungo Thabani Kamusoko na kupanguliwa vema kipa machachari Aishi Manula.