BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC na Taifa Stars, Shomari Kapombe, leo amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) mwezi Januari mwaka huu.

Nyota huyo wa Azam FC alifanikiwa kucheza mechi mbili kati ya tatu dhidi ya African Sports aliyotoa pasi ya mwisho ya bao la Frank Domayo, mchezo ulioisha kwa sare ya bao 1-1 na ile ya Mgambo JKT, aliyofunga mabao mawili ya mabingwa hao yaliyowapa ushindi wa 2-1 ndani ya Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Washindani wa Kapombe kwenye kinyang’anyiro hicho katika mwezi huo, walikuwa mshambuliaji wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Jeremiah Juma na beki wa Coastal Union ya Tanga, Miraji Adam.

Kwa kutwaa tuzo hiyo, Kapombe atazawadiwa kitita cha Sh. milioni moja na wadhamini wa ligi hiyo Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Limited.

Kapombe anasema nini?

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz jioni ya leo Kapombe alisema kuwa cha kwanza anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye ndiye amemfanya aweze kutwaa tuzo hiyo.

“Lakini pia napenda kuishukuru timu ya Azam ambayo ndio imenifanya niweze kuwa bora na kuonekana bora bila kusahau pia nawashukuru wachezaji wenzangu na wao wamenifanya mimi niweze kuwa bora na niweze kuchaguliwa kuwa mchezaji bora mwezi Januari,” alisema.

Kapombe alisema ameipokea tuzo hiyo kama changamoto, ambayo inaweza kumfanya kuendelea kufanya vizuri katika ligi, timu yake pamoja na kuisaidia Azam FC.

“Napenda kuonekana kuwa bora kwa sababu naisaidia timu yangu katika kufikia malengo fulani, kwa hiyo mimi mwenyewe nina malengo yangu niliyojiwekea, ninachoshukuru ni moja kama hivyo natwaa tuzo ya mchezaji bora, lakini nadhani yapo malengo makubwa zaidi yapo mbeleni, namuomba Mwenyenzi Mungu anipe uhai, anipe nguvu ili niweze kuyafanikisha,” alisema.

Siri ya mafanikio yake?

“Cha kwanza mimi naweza kusema siri kubwa ya mimi kufanikiwa ni kujituma nje na ndani ya uwanja, cha pili kumsikiliza kocha anasemaje na anahitaji nini, cha tatu ni kuwa na mahusiano mazuri na wachezaji wenzangu na cha nne ni kujitolea uwanjani ili kuifanya timu yangu ifike sehemu nzuri na mimi kuonekana niko bora zaidi,” alisema beki huyo wa zamani wa Simba, AS Cannes ya Ufaransa.

Anachowaambia mashabiki wa Azam FC?

Kapombe aliwaomba mashabiki wa Azam FC waendelee kuipa sapoti timu hiyo pamoja na yeye binafsi ili aweze kuitumikia timu kwa nguvu na kwa moyo mmoja.

“Kwa sababu mimi naipenda timu ya Azam na nawapenda mashabiki wote na napenda kuwaambia kuwa waendelee kuipa sapoti timu yao mpaka lifikie lile lengo ambalo tumejiwekea,” alisema.

Amefanya nini msimu huu?

Kapombe anayesifika kwa soka la kasi akipanda na kushuka katika majukumu yake ya ulinzi upande wa kulia na wakati mwingine kushoto, mbali na kufanikiwa kutoa pasi nyingi za mwisho msimu huu pia amefunga mabao saba kwenye ligi mpaka sasa.

Hilo limemfanya kuwa beki pekee kufunga mabao mengi kwenye ligi hiyo huku akiwa mmoja wa wafungaji bora ndani ya Azam FC msimu huu, akizidiwa na Kipre Tchetche aliyefunga tisa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyetupia nane mpaka sasa.