KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kesho saa 10 jioni inatarajia kuendeleza kampeni ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), pale itakapomenyana na wenyeji wao, Panone ndani ya Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Mchezo huo wa raundi ya 16 bora ya michuano hiyo, unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka mkoani Kilimanjaro, wengi wao wakitaka kuiona kwa mara ya kwanza Azam FC ikicheza mjini hapo.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya Azam FC kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Stewart Hall, alisema wamekuja na lengo moja tu la kushinda mechi hiyo huku akidai kuwa anatarajia kumtumia straika wake, Didier Kavumbagu, aliyekuwa nje ya dimba kwa takribani miezi miwili akiuguza majeraha ya enka.

“Tumekuja hapa kushinda na hakuna kitu kingine na hii ni kwa kuwa tunautaka ubingwa wa FA, maandalizi yetu tayari yamekamilika, tumekuja na kikosi imara cha wachezaji 22 na hii yote ni kukamilisha lengo letu la kushinda…Nashukuru hivi sasa Kavumbagu yupo fiti na yupo katika mipango ya mechi hiyo,” alisema.

Kikosi cha Azam FC mara baada ya kuwasili ndani ya Uwanja wa Ndege wa KIA saa 6 mchana, kilienda moja kwa moja kambini mkoani Arusha na kufikia katika Hoteli ya City Link.

“Tumeamua kuja kuweka kambi Arusha kutokana na ugumu ndani ya mji wa Moshi na hii imechangiwa na  michuano ya Kilimanjaro Marathon, kuna wageni wengi hivi sasa Moshi ikizingatiwa ni mji mdogo, hivyo isingekuwa rahisi kwetu kukaa pale. Arusha tumepata eneo zuri la kupumzika na amani pamoja na la usiri,” alisema.

Hall alizungumzia aina ya uwanja watakaoenda kuchezea mjini Moshi (Ushirika) na kusema kuwa: “Tunatarajia uwanja tutakaochezea utakuwa ni mbovu, mimi sijauona bado ila nimepata ripoti, pia hatujapata nafasi ya kufanyia mazoezi kwenye uwanja huo siku moja kabla ya mechi kama inavyotakiwa na hii ni kutokana na Kilimanjaro Marathon, hili ni tatizo.”

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB ilifuzu kwa hatua hiyo baada ya kuichapa Afrian Lyon mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, yaliyofungwa na Farid Mussa, aliyefunga mawili huku Mudathir Yahya na Ame Ally wakipiga moja kila mmoja.

Panone FC yenyewe inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) na kufundishwa na kocha mkongwe mzawa, Fred Felix Minziro, iliitoa timu ya Madini ya mkoani Arusha 3-1, mchezo uliopigwa ndani ya Uwanja wa Ushirika.

Mshindi wa mchezo huo atafuzu moja kwa moja kwa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, ambayo kwa mwaka huu ndio itakayotoa mwakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.