KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa suluhu waliyoipata dhidi ya Tanzania Prisons sio majanga kwa sababu bado wapo kwenye vita ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Suluhu hiyo imeifanya Azam FC kuvuna pointi nne kati ya sita jijini Mbeya baada ya awali kuichapa Mbeya City mabao 3-0 na sasa inabanana kileleni na Yanga ikiwa katika nafasi ya pili wakijikusanyia jumla ya pointi 46 sawa na Yanga inayoongoza, zote zikizidiwa mchezo mmoja na Simba inayoshika nafasi ya tatu (45).

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Hall amesema kuwa sio majanga kwani bado wanao mchezo mmoja mkononi dhidi ya Simba na wamelingana pointi na Yanga ambao watacheza nao kwenye mechi ijayo itakayofanyika Machi 5, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.  

Hali ya mchezo na mwamuzi?

“Prisons ni timu inayotumia nguvu sana, walifanya rafu kadhaa mbaya nyingine kwa viwiko na wakati mwingine tukiwa hatuna mpira, nadhani mwamuzi hakuwa na ubora unaotakiwa, mwamuzi angeweza kuwapa kadi za njano mapema wachezaji na Prisons ili kutuliza aina ya uchezaji wao, lakini hakufanya hivyo.

“Tulijitahidi kama timu kucheza kwa nguvu, tulipambana kwa nguvu sana kusaka ushindi…Hakuna aliyeshinda hapa, Simba alikuja alifungwa (1-0), Yanga naye alilazimusha sare dakika za mwisho kwa kupewa penalti (2-2),” alisema Hall.

Hall alisema walifanikiwa kutengeneza nafasi mbili hadi tatu kipindi cha kwanza, lakini zilishindwa kuzaa mabao baada ya mojawapo Kipre Tchetche kugongesha mwamba na nyingine Prisons wakiokoa kwenye mstari wa goli.

“Pia tulinyimwa penalti ya wazi baada ya Kapombe (Shomari) kuangushwa ndani ya eneo la 18, hivyo tungeweza kuinaliza mechi ndani ya kipinfdi cha kwanza kwa kushinda, lakini tulishindwa, kipindi cha pili walipoteza sana muda, hawakuwa na nia ya kushinda na walitumia kila mbinu kutuzuia tusishinde,” alisema.

Mwingereza huyo hakusita kuelezea tatizo lililoikabili timu yake kwenye mchezo huo baada ya kudai kuwa, walishindwa kupiga pasi nzuri za mwisho, krosi nzuri, mashuti na vichwa vizuri kila walipokaribia eneo la 18 (penalty area), jambo ambalo liliwapa urahisi wapinzani wao kuwazuia.

Kadi ya njano ya Erasto Nyoni?

Beki wa kati wa Azam FC kupitia mfumo wa 3-5-2, Erasto Nyoni, alipewa kadi ya njano kwenye mchezo huo kwa kumfuata mchezaji mmoja wa Tanzania Prisons na kuanza kukoromeana naye pamoja na kutaka kusukumana.

Kadi hiyo inamfanya Nyoni ambaye yupo kwenye kiwango bora kabisa hivi sasa kama ilivyo kwa David Mwantika kwenye eneo la ulinzi, kuikosa mechi ijayo ya ligi dhidi ya Yanga.

Hall ameonekana kuchukizwa sana na kadi hiyo, akidai kuwa Nyoni alipata kadi ya kizembe sana na ambayo angeweza kuiepuka.

“Niliongea na wachezaji kuhusiana na aina ya kadi hizo kabla ya mchezo, lakini nimeshangaa kutokea na sasa ataikosa mechi ya Yanga, hadi sasa Nyoni amecheza vema sana akiwa na mabeki wengine wawili wa kati Pascal Wawa na David Mwantika, ndani ya mechi mbili zilizopita hatujaruhusu bao, sasa nalazimika kubadilisha safu hiyo kuelekea mechi hiyo, na jambo la kumshukuru Mungu Aggrey Morris anarejea.

Baada ya kuona hali hiyo, nililazimika kumtoa John Bocco ili kumwepusha asikose mechi ya Yanga, hasa baada ya kuona kuwa kuna kila dalili za mwamuzi kumpa kadi ya njano,” alisema.

Azam FC yawasili Dar kwa mwewe

Wakati huo huo, kikosi cha Azam FC kimeshawasili jijini  Dar es Salaam saa 3 asubuhi hii kwa usafiri wa ndege ya Fast Jet ikitokea jijini Mbeya.

Kikosi hicho cha Azam FC kinachodhaminiwa na Benki ya NMB, kitarejea mazoezini kesho kwenye viunga vya Azam Complex na kuingia kambini moja kwa moja tayari kabisa kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Panone ya jijini Moshi, utakaofanyika Uwanja wa Ushirika Jumatatu ijayo (Februari 29).

Mchezo huo uliotakiwa kufanyika Jumapili ijayo (Februari 28), umesogezwa siku moja mbele kufuatia Uwanja wa Ushiriki kutumika kwa shughuli za mbio za ‘Kilimanjaro Marathon’ siku hiyo.