KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imezidi kuisogelea Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kutoa suluhu dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jiini Mbeya jioni ya leo.

Matokeo hayo yameifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 46 sawa na Yanga, lakini imebakia katika nafasi ya pili baada ya kuzidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku Simba iliyojikusanyia pointi 45 ikiwa nafasi ya tatu.

Lakini Azam FC na Yanga zimebakiwa na mechi moja za mkononi dhidi ya Simba, zote zikiwa kwenye vita kubwa ya kuwania ubingwa wa ligi msimu huu.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa kwa pande zote mbili na iliwachukua dakika 10 tu Azam FC kuweza kupata kona takribani nne, ikashindwa kuzitumia vema zote na moja kati ya hizo kwenye dakika ya sita ingeweza kuipatia bao.

Hiyo ilitokana na kona iliyochongwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ kumkuta Kipre Tchetche aliyepiga kichwa safi kilichookolewa kwenye mstari wa goli na mabeki wa Tanzania Prisons.

Azam FC ingeweza kupata mkwaju wa penalti dakika ya 15 baada ya beki Shomari Kapombe kuangushwa kwenye eneo la hatari na mabeki wa Prisons, lakini mwamuzi aliikataa na kuamua ipigwe kona kuelekea lango la maafande hao, ambayo hata hivyo haikuweza kuzaa matunda.

Katika kipindi chote cha kwanza, Azam FC ilionekana kumiliki mpira lakini tatizo kubwa lilionekana kwenye utengenezaji wa nafasi na hii ni baada ya Tanzania Prisons kujirundika langoni mwao kila Azam FC ilipokuwa ikishambulia.

Hata kipindi cha pili, Tanzania Prisons iliendelea na mchezo wao huo na Azam FC ililazimika kufanya mabadiliko dakika ya 63 kwa kutoka kiungo Michael Bolou aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Farid Mussa.

Kuingia kwa Farid kulimlazimu Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, kubadili mbinu za uchezaji kwa kumrudisha katikati kwenye kiungo wa ushambuliaji Messi na Farid kuhamia upande wa kushoto aliokuwa akicheza winga huyo.

Kuelekea dakika za mwisho, Tanzania Prisons ilinekana wazi ikihitaji suluhu hasa baada ya kucheza soka la kupoteza muda kwa wachezaji wake kujiangusha mara kwa mara huku mwamuzi akishindwa kuwachukulia hatua zozote.

Azam FC ilifanya mabadiliko mengine dakika ya 88 kwa kutoka nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na nafasi yake kuchukuliwa na Allan Wanga, mabadiliko hayo yalifanya ili kumlinda nahodha huyo asipate kadi ya njano.

Baada ya kumalizika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaanza safari kesho asubuhi kwa usafiri wa ndege ya Fast Jet kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Panone utakaofanyika Jumatatu ijayo (Februari 29) ndani ya Uwanja wa Ushirika jijini Moshi.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, David Mwantika, Ramadhan Singano ‘Messi’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Jean Mugiraneza ‘Migi’, Michael Bolou/Farid Mussa dk63, John Bocco/Allan Wanga dk88 na Kipre Tchetche.