KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendeleza rekodi yake nzuri ya kuitambia Mbeya City, baada ya kuichapa mabao 3-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Hiyo inakuwa mechi ya nne ya ligi kwa Azam FC kushinda dhidi ya Mbeya katika mechi sita walizokutana, ambapo mbili nyingine zimeisha kwa sare, zote zikiwa ndani ya Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Jambo la kuvutia zaidi washambuliaji wa Azam FC, nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Tchetche, ambao wanaongoza kufunga mabao mengi dhidi ya Mbeya City kila mmoja akifunga mawili, leo pia walijiongezea idadi baada ya kila mmoja kufunga bao moja kwenye ushindi huo mnono wa mabingwa hao.

Tchetche ndiye aliyeanza kuiweka mbele Azam FC kwa bao safi la kichwa dakika 41 akiunganisha kona iliyochongwa na kiungo Himid Mao ‘Ninja’, ambalo liliwapunguza kasi Mbeya City waliokuwa wakionekana kucheza vema kipindi cha kwanza.

Bao hilo lilidumu hadi kinamalizika kipindi cha kwanza, ambapo Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alikiongezea nguvu kikosi chake kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya kumtoa kiungo Mudathir Yahya na kuingia winga Farid Mussa.

Mabadiliko hayo yalimlazimu Kocha Hall kumbadilisha namba Ramaadhan Singano ‘Messi’ aliyeendeleza kiwango chake bora leo, kutoka winga wa kushoto kumpisha Farid na kupewa majukumu mapya ya kucheza kama kiungo wa ushambuliaji anayetokea katikati ya uwanja.

Azam FC ilionekana kucheza vema kipindi cha pili kwa kuwabana vilivyo Mbeya City waliokuwa wakiongozwa na wachezaji wakongwe viungo Haruna Moshi ‘Boban’, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na kipa Juma Kaseja.

Alikuwa ni nahodha Bocco, aliyeihakikishia ushindi Azam FC kwa kufunga bao zuri la kuserereka chini dakika ya 63 akimalizia pasi safi ya Shomari Kapombe ambayo ilimshinda kipa Juma Kaseja aliyeteleza kabla ya Bocco kuuwahi mpira na kuuweka nyavuni.

Dakika ya 74 Hall alimpumzisha nahodha msaidizi wa Azam FC, Himid akihofia kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya njano kwenye kipindi cha kwanza na nafasi yake ilichukuliwa na Frank Domayo ‘Chumvi’, pia alimtoa Tchetche dakika ya 81 na kuingia Ame Ally.  

Kasi ya Azam FC ya kusaka mabao zaidi ilizidi kuwachanganya Mbeya City dakika ya 84 baada ya kipa wao Kaseja kujikuta akiiokoa vibaya krosi ya Messi na kuutema vibaya mpira uliomkuta Farid aliyepiga shuti zuri lililojaa kimiani na kuiandikia timu yake bao la tatu.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB ililazimika kutumia jezi mbili tofauti kwenye mchezo huo, kipindi cha kwanza (dark blue) na kipindi cha pili nyeupe kutokana jezi kuloa kufuatia mvua iliyonyesha sana kipindi cha kwanza na kufanya jezi za timu zote kushabihiana.

Hadi dakika 90 za mchezo huo zimalizika, Azam FC ilijihakiiishia kuondoka na pointi zote tatu, zilizoifanya kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 45 sawa na Simba, lakini inazidiwa michezo miwili na wekundu hao na mmoja dhidi ya Yanga iliyoko kileleni kwa pointi 46.

Azam FC ina nafasi kubwa ya kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi Jumatano ijayo (Februari 24), endapo itaifunga Tanzania Prisons katika mechi yake ya kwanza ya kiporo itakayofanyika ndani ya Uwanja wa Sokoine jijini hapa Mbeya.

Kikosi cha Azam FC leo;

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Ramadhan Singano ‘Messi’, David Mwantika, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Jean Mugiraneza ‘Migi’, Himid Mao ‘Ninja’ dk 74, Mudathir Yahya/Farid Mussa dk 45, John Bocco (C), Kipre Tchetche/Ame Ally dk 81