ZIKIWA zimesalia saa kadhaa kabla ya kuanza kwa mchezo kati ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC na wenyeji wao Mbeya City, mechi hiyo imekuwa ikizungumziwa na mashabiki wengi jijini hapa Mbeya.

Azam FC imetua jijini Mbeya ikiwa na mkakati wa kuondoka na pointi zote sita, tatu za leo saa 10.00 jioni dhidi ya Mbeya City na tatu nyingine watakapoivaa Tanzania Prisons Jumatano ijayo (Februari 24), ili kuzidisha mbio za kuwania taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Ili kuashiria kutakuwa na mchezo mkali leo, kila upande umeonekana kumtambia mwenzake, kama hiyo haitoshi kwa upande wa mashabiki, baadhi yao wameonekana kuitambia huku wengine wakiishangilia na kuipungia mikono kila basi la Azam FC lilipokuwa likipita jijini hapa (Mbeya).

Hata kwenye mazoezi ya Azam FC jana jioni, mashabiki kadhaa walishindwa kujizuia na kuamua kujitokeza kwa wingi kuyashuhudia na kukaa jukwaa la VIP katika Uwanja wa Sokoine, ambao ndio utatumika kwa ajili ya mechi hizo mbili za matajiri hao wa Azam Complex.

Tayari nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, ameshawatoa hofu mashabiki wa timu hiyo akiwaambia kuwa wamesahau ya nyuma yaliyopita na sasa wanapambana kuhakikisha wanashinda mechi hizo mbili na kuondoka na pointi sita zote jijini Mbeya.

Hata Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa wamejipanga kuzoa pointi zote tatu katika mchezo huo licha ya ugumu watakaokutana nao.

Mwingereza huyo, amesema anatarajia kuwakosa wachezaji wake watano, mshambuliaji Didier Kavumbagu, mabeki Aggrey Morris, Abdallah Kheri na Racine Diouf walio majeruhi, huku kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, akiondolewa kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kukusanya kadi tatu za njano.

Nafasi ya Sure Boy itachukuliwa na kiungo Mudathir Yahya huku pia Hall akieleza kuwa anatarajia kumwanzisha winga wa kushoto Ramadhan Singano ‘Messi’ kuchukua nafasi ya kinda machachari Farid Mussa.

Azam FC itaingia uwanjani leo kupambana na Mbeya City ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union (1-0), uliohitimisha rekodi yao ya kutofugwa mechi yoyote ya ligi tokea Mei 2, mwaka jana ilipofungwa mara ya mwisho na Simba mabao 2-1.

Mbeya City yenyewe inayofundishwa na kocha mpya raia wa Malawi, Kinnah Phiri, imetoka kuichapa Toto Africans ya Mwanza mabao 5-1, uliofanyika jijini hapa.

Ushindi wowote wa Azam FC utaifanya kufikisha jumla ya pointi 45 na kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kama mtanange kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga utaisha kwa sare ya aina yoyote ile au Yanga kupoteza mchezo huo, vilevile itakuwa imejitengenezea njia ya kurejea kileleni Jumatano ijayo endapo wataifunga Tanzania Prisons.

Lakini ikimbukwe kuwa mpaka sasa Azam FC ina viporo vya mechi mbili dhidi ya Simba inayongoza kwa pointi 45 na kimoja dhidi ya Yanga iliyo nafasi ya pili kwa kujisanyia jumla ya pointi 43.

REKODI ZAO VPL (HEAD TO HEAD)

Mchezo huo wa leo utakuwa ni wa sita kwa timu hizo kukutana tokea kupanda daraja kwa Mbeya City msimu wa 2013/14, ambapo Azam FC imepata matokeo mazuri ya asilimia 100 dhidi yao kwa kipindi chote hicho.

Rekodi inaonyesha kuwa Azam FC imeshinda mechi tatu, mbili zikiwa katika uwanja wanaochezea leo wa Sokoine ikiwemo ile iliyowapa taji la ligi 2013/14 na mmoja Azam Complex, huku zikitoka sare mbili (3-3, 1-1) ndani ya Azam Complex.

Ushindi wa mabao 2-1 wa Azam FC kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huu yaliyofungwa na Kipre Tchetche na Mudathir Yahya, iliipa rekodi matajiri hao ya kushinda mechi ya kwanza dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Azam Complex baada ya mechi zote za awali kuisha kwa sare.

Mpaka sasa kwenye rekodi aliyekuwa mshambuliaji wa Mbeya City, Mwagane Yeya, ndiye anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye mpambano baina ya timu hizo, akifunga manne, matatu akifunga kwa staili ya hat-trick katika sare ya 3-3 Azam Complex (2013/14).

Kwa upande wa Azam FC wanaoongoza kuifunga mabao mengi Mbeya City ni nahodha John Bocco aliyetupia mawili sawa na Muivory Coast Kipre Tchetche, ambao wote leo wataongoza mashambulizi ya mabingwa hao kusaka pointi muhimu.

Takwimu za ufungaji mabao zinaonyesha kuwa jumla ya mabao 15 yamefungwa kwenye mechi zote hizo, Azam FC ikifunga tisa na sita yakitupiwa na Mbeya City.