KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, inatarajia kuandika rekodi mpya saa chache zijazo ya kufikisha jumla ya mashabiki 300,000 wanaofuatilia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook (unaojulikana kama Azam FC).

Wakati Azam FC tukiwa tunashikilia ubingwa wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), pia klabu hiyo ndio inayoongoza kufuatiliwa na mashabiki wengi facebook kwa upande wa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla, hadi sasa ukurasa wake unatembelewa na jumla ya mashabiki 299,927 (like’s), wakisalia 73 tu kufikia 300,000.

Kama hiyo haitoshi, Azam FC ni miongoni mwa timu 30 zenye ukurasa wa facebook wenye mashabiki wengi zaidi barani Afrika, ambapo kwa Afrika Mashariki na Kati inayowafuatia ni mabingwa wa nchini Kenye, Gor Mahia wenye ‘likes’ 251,437 hadi kufikia leo asubuhi.

Azam FC tunapenda kuwashukuru mashabiki ambao mmeendelea kuwa wadau wetu wakubwa tokea tulipoanza utaratibu huu wa kisasa zaidi katika kutoa habari zetu na pia tusingependa kusita kuwapongeza kwa michango yenu ya mawazo mnayoendelea kutoa kwenye ukurasa wetu huo kwani mmekuwa mkitusaidia kurekebisha baadhi ya mambo.

Ingawa ukurasa wetu unaelekea kufikisha mashabiki 300,000, habari zetu za Azam FC zinawafikia mashabiki wengi zaidi ya hao kwani namna mfumo wa facebook ulivyo, habari zetu zinaonwa zaidi na marafiki wa mashabiki wetu pale wanapotembelea ukurasa wao na hivyo watu wengi zaidi kupata fursa ya kujua kinachoendelea katika klabu yetu.

Kutokana na mafanikio hayo tunayoendelea kuyapata, bado tuna mipango kabambe ya kufikisha jumla ya mashabiki 400,000 kwenye ukurasa wetu hadi mwishoni mwa mwaka huu, hivyo ukiwa kama mshabiki tulioanza wote safari hii tunahitaji ushirikiano wako kwenye hilo.

Namna pekee ya wewe kushirikiana nasi kwenye kampeni hii ni kila mshabiki kumshawishi ndugu, jamaa au rafiki yake ku-like ukurasa wetu kuanzia sasa, hivyo ikiwa tutafanya kazi kwa ushirikiano tunaweza kuvuka lengo kwa kuwa na mashabiki wengi zaidi.

Tunaamini ya kuwa si kila walio-like ukurasa wetu ni mashabiki wetu, lakini hilo halijalishi kwani tunachoamini sisi ni kuwa katika mipango yetu ya kuleta mapinduzi ya kweli kwenye soka la Tanzania kama ilivyo adhma yetu tokea kuanzishwa kwa klabu hii, mashabiki wa aina yoyote ile ni muhimu kwetu na tunaomba muendelee kutuunga mkono katika safari yetu hii ndefu tuliyoianza.

Mwisho tungependa mashabiki wetu mtambue ya kuwa kama lilivyo lengo letu la Azam FC kuwa klabu bora barani Afrika, mipango yetu mingine tuliyojiwekea ni kuwa klabu iliyojizolea mashabiki wengi kwenye mitandao ya kijamii na pia uwanjani.

Azam FC;

TIMU BORA, BIDHAA BORA