KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kushuka dimbani kesho saa 10.00 jioni kwenye Uwanja Mkwakwani, Tanga kuvaana na wenyeji wao, Coastal Union katika mchezo wa raundi ya 18 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wakazi wengi wa mkoani Tanga, unatarajia kuwa mkali kutoka na rekodi za timu zote mbili, ambapo Azam FC itaingia dimbani ikiwa inataka kuendeleza rekodi ya kutofungwa mchezo wowote wa ligi mpaka sasa.

Rekodi hiyo imeendelea kuwaweka kwenye hatua nzuri mabingwa hao wa Kombe la Kagame kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu hasa ikizingatiwa ya kuwa mpaka sasa imeshajikusanyia jumla ya pointi 42 katika nafasi ya tatu, ikizidiwa mechi tatu za kucheza na kinara Simba mwenye pointi 45 na mechi mbili dhidi ya Yanga inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 43.

Kuelekea mchezo huo, kitakwimu Azam FC ina rekodi nzuri dhidi ya Wagosi wa Kaya hao kwani katika mechi zote tisa walizokutana kwenye ligi, Azam FC imeshida saba na mbili zikiisha kwa sare na haijawahi kufungwa mechi yoyote.

Katika mechi zote hizo tisa jumla ya mabao 21 yamefungwa, ambapo Azam FC imefunga asilimia 98 ya mabao yote ikitupia 18 na Coastal ikifunga matatu pekee.

Azam FC itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi kwenye mchezo uliopita wa ligi kwa kuifunga Mwadui wa Shinyanga bao 1-0, lililofungwa na straika hatari Kipre Tchetche huku Coastal Union ikipigwa na Toto Africans mabao 2-0.

Ndani ya mechi tano zilizopita za ligi za timu zote mbili, Azam FC imeshinda jumla ya mechi nne na kutoka sare mmoja walipocheza na African Sports (1-0), huku Coastal Union ikiwa na matokeo mabaya ya kufungwa mechi tatu, ikiambulia sare moja na kushinda moja pia dhidi ya Yanga (2-0)

Coastal Union iliyojikusanyia jumla ya 13 katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, mabao yaliyofungwa na Shomari Kapombe na Kipre Tchetche.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, msimu huu pia imekuwa na rekodi nzuri ya mechi za ugenini kuliko timu nyingine yoyote hadi sasa, ambapo imecheza mechi saba ugenini, ikishinda sita na kutoa sare mchezo mmoja dhidi ya Yanga (1-1) katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kitakwimu imekusanya pointi 19 ugenini kati ya 21 ilizotakiwa kuzipata.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema anajua mchezo huo utakuwa mgumu lakini ni lazima washinde ili kuendelea kuwapa presha wapinzani wao Simba na Yanga kwenye mbio za ubingwa.

Hall amesema kuwa bado ataendelea kutumia mbinu zake zile zile anapocheza mechi za ugenini hasa kwenye uwanja mbovu kama Mkwakwani, ambapo moja ya mbinu kubwa anayotumia na kumpatia mafanikio ni kucheza kwa kutumia mipira ya juu na kuwatumia wachezaji wenye nguvu na wanaomudu viwanja vibovu.

Katika hatua nyingine alisema atawakosa mabeki wake wanne wa kati Abdallah Kheri, David Mwantika, Racine Diouf na Aggrey Morris kipa Mwadini Ally na mshambuliaji Didier Kavumbagu, ambao ni majeruhi.