KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC ina rekodi ya asilimia 100 ya kutopoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Coastal Union.

Azam FC inatarajia kumenyana na Coastal Union Jumapili hii (Februari 14) katika mchezo wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kwa mujibu wa takwimu za ligi hiyo tokea Azam FC ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/2009, zinaonyesha kuwa imekutana mara tisa na Coastal Union kwenye mechi za ligi, ikishinda mara saba na kutoka sare mbili.

Katika mechi hizo, zilizochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani ni nne pekee, ambapo Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB imeshinda mbili (1-0, 1-0) na nyingine mbili zikiisha kwa sare (0-0, 1-1), huku Azam FC ikishinda mechi tano zote zilizochezwa Azam Complex.

Jumla ya mabao 21 yamefungwa kwenye mechi hizo zote tisa, ambapo Azam FC imefunga asilimia 98 ya mabao yote ikitupia 18 na Coastal ikifunga matatu pekee.

Azam FC pia Julai mwaka jana ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Coastal Union pamoja na African Sports kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame, na ikawachapa Wagosi wa Kaya hao bao 1-0, lililofungwa na Ame Ally.

Kuelekea mchezo wa Jumapili hii, tayari Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, ameweka wazi kuwa anataka kuendeleza rekodi waliyoweka ya kufanya vizuri kwenye mechi za ugenini msimu huu pamoja na ile waliyonayo ya kufanya vema katika Uwanja wa Mkwakwani.

Azam FC ambayo ni miongoni mwa timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, mpaka sasa ndio timu pekee iliyokuwa na rekodi ya kutopoteza mchezo wowote wa ligi katika mechi 16 walizocheza, ikishinda 13 na sare tatu ikijikusanyia jumla ya pointi 42 sawa na Simba iliyo nafasi ya pili huku ikizidiwa pointi moja tu na Yanga inayoongoza ligi kwa pointi 43.

Lakini matajiri hao wa Azam Complex wana mechi mbili mkononi, zinazoweza kuwaweka juu kileleni kwa tofauti ya pointi tano kwa atakayemfuatia kama ikizishinda zote.

REKODI AZAM FC V COASTAL UNION

2011/2012

Coastal Union 0-1 Azam FC (Septemba 21, 2011)

Azam FC 3-0 Coastal Union (Machi 07, 2012)

2012/2013

Azam FC 4-1 Coastal Union (Novemba 01, 2012)

Coastal Union 1-1 Azam FC (Aprili 26, 2013)

2013/2014

Coastal Union 0-0 Azam FC (Oktoba 05, 2013)

Azam FC 4-0 Coastal Union (Machi 15, 2014)

2014/2015

Azam FC 2-1 Coastal Union (Novemba 08, 2014)

Coastal Union 0-1 Azam FC (Machi 22, 2015)

2015/2016

Azam FC 2-0 Coastal Union (Septemba 30, 2015)

Coastal Union ?-? Azam FC (Februari 14, 2016)