KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imepangwa kucheza na timu ya Panone kutoka mkoani Kilimanjaro katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Droo hiyo ya raundi ya nne iliyotolewa leo mchana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeonyesha kuwa, Azam FC itacheza ugenini mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi Februari 28 mwaka huu.

Huo ni mchezo wa pili wa Azam FC kwenye michuano hiyo, ilianza kwa kuichapa African Lyon mabao 4-0 Januari 25 mwaka huu ikicheza tena ugenini katika mechi ya raundi ya 32 bora.

Panone FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na kufundishwa na kocha mkongwe mzawa, Fred Felix Minziro, ilifika hatua hiyo kwa kuitandika timu ya Madini ya mkoani Arusha maba 3-1 katika Uwanja wa Ushirika.

Mabao ya Azam FC katika mtanange huo uliofanyika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, yalifungwa na Farid Mussa, aliyetupia mawili huku Mudathir Yahya na Ame Ally wakipiga moja kila mmoja.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB ikivuka tena mtihani huo itaingia moja kwa moja hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Ratiba kamili 16 bora:

Ijumaa, Februari 26

Ndanda FC vs JKT Ruvu (Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara)

Coastal Union vs Mtibwa Sugar (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga)

Jumamosi, Februari 27

Mwadui FC vs Rhino Rangers (Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga)

Tanzania Prisons vs Mbeya City/Wenda FC (Uwanja wa Sokoine, Mbeya)

Jumapili, Februari 28

Panone FC vs Azam FC (Uwanja wa Ushirika, Moshi)

Simba SC vs Singida United (Uwanja wa Taifa, Dar)

Toto African vs Geita Gold (Uwanja wa Kirumba, Mwanza)

Jumanne, Machi 1

Young Africans vs JKT Mlale (Uwanja wa Taifa, Dar)