KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuwa mwenyeji wa michuano maalumu ya kimataifa ya timu nne itakayofanyika mwanzoni mwa mwakani.

Michuano hiyo ni ile waliyoenda kushiriki jijini Ndola Zambia hivi karibuni na kutwaa ubingwa, ambapo imeanzishwa kwa muungano wa klabu tatu, Azam FC, TP Mazembe na Zesco United.

Akizungumza hivi karibuni na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya kikosi hicho kurejea kutoka Zambia, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema mwakani ni zamu yao kuandaa michuano hiyo na hivi sasa wanajipanga  kuweza kuwaalika marafiki zao hao pamoja na kuangalia namna gani watakavyocheza nao hapa nyumbani.

“Tulialikwa kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo ilipofanyika Kongo katika mji wa Lubumbashi, ambapo tulikubaliana kimaandishi kwamba tutengeneze umoja huu, ambao ni umoja wa vilabu vitatu TP Mazembe, Zesco United na sisi Azam FC.

“Na mwaka huu tumepata nafasi hiyo tena kwa kualikwa, ambapo tumeweza kuwa mabingwa na mwaka jana TP Mazembe walikuwa mabingwa na akaenda kuchukua ubingwa wa Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika), kwa hiyo Azam FC mwaka huu tumechukua ubingwa tunategemea kupata matokeo mazuri katika mashindano ya CAF kwa sababu mechi nzuri na tumejiandaa,” alisema.

Kawemba alisema kuwa lengo kubwa la kuunda umoja huo ni kuweza kuzipa nafasi timu zinazoshiriki michuano ya CAF kuweza kufanya mazoezi kwa pamoja, huku akisisitiza kuwa michuano ya umoja huo ni mikubwa na sio kama wengi wanavyodhania.

“Ingawa watu wanaona kuwa hayana tija, lakini kwetu tunaamini ya kuwa yanatija na yametupa nafasi hiyo ya kujijenga, kila mtu aliona tulivyocheza mwaka jana dhidi ya El Merreikh baada ya kutoka Lubumbashi na mwaka huu tunaamini kabisa mechi ya Bidvest Wits itakuwa tofauti na tulikuwa tukisema hivyo pia hata hao wanaotubeza sasa hivi walikuwa wakituuliza Azam mnajiandaa kwa namna gani kwenye michuano ya Kimataifa, kwa hiyo haya ndio majibu na huwa hatuzungumzi bali tunafanya kwa vitendo,” alisema.

Aliongeza kuwa; “Na sio kama tunabeza mtu yoyote, hatuwezi kujiandaa kucheza dhidi ya Bidvest kwa kucheza na klabu ya hapa nyumbani, hakuna klabu yoyote inayoweza kutupa mazoezi hapa, kwa hiyo tumeenda kufanya mazoezi huko kwa ajili ya Bidvest na timu zinazokuja na kwa hapa nyumbani tumerudi, tumefanya mazoezi ya juu kidogo na tunaamini hakutakuwa na tatizo lolote.”

Bosi huyo aliwaondoa hofu mashabiki wa Azam FC kwa kuwaambia kuwa wamekuja kuendeleza pale walipoishia na hawana wasiwasi kwa yanayoendelea hivi sasa Tanzania katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

“Tunaangalia michezo yetu iliyoko mbele yetu na tuna uhakika tutafanya vizuri na tutakaa katika nafasi ambayo tunastahili kukaa na kila mtu anajua nafasi hiyo ni ipi,” alimalizia Kawemba.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB hivi sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejisanyia jumla ya pointi 42 sawa na Simba inayokamata nafasi ya pili na Yanga inayoshika usukani kwa pointi 43.

Lakini matajiri hao wa Azam Complex wana mechi mbili mkononi, zinazoweza kuwaweka juu kileleni kwa tofauti ya pointi tano kwa atakayemfuatia kama wakizishinda zote, jambo la kuvutia zaidi mpaka sasa ndio timu pekee kwenye ligi ambayo haijapoteza mchezo wowote.