KINDA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Bryson Raphael, amezidi kuing’arisha timu ya Ndanda kutoka Mtwara, anayoichezea kwa mkopo baada ya kufunga bao dhidi ya Mtibwa Sugar, lililowapa sare ya bao 1-1 ugenini (Uwanja wa Manungu).

Azam FC ilifanya uamuzi wa kumtoa kwa mkopo kiungo huyo kwenye usajili wa dirisha dogo Desemba mwaka jana, sambamba na wachezaji wengine chipukizi beki Ismail Gambo ‘Kusi’ (Mwadui), kiungo Omary Wayne (Coastal Union) na straika Kelvin Friday (Mtibwa Sugar).

Bryson, 19, amekuwa ni mchezaji wa kutegemewa wa Ndanda tokea asajiliwe na kikosi hicho, ambapo hilo ni bao lake la pili kwenye mbili mfululizo, jingine alilifunga Alhamisi iliyopita walipoilaza Coastal Union bao 1-0 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Ndanda kupata pointi hizo nne kumeifanya Ndanda izishushe chini Majimaji na Mgambo JKT baada ya kufikisha jumla ya pointi 17 sawa na maafande hao kutoka mkoani Tanga.

Kinda mwingine wa Azam FC aliyekuwepo kwa mkopo Mtibwa Sugar, Friday naye Jumatano iliyopita alionyesha cheche zake kwa kufunga moja ya mabao walipolazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya Toto Africans.

Wachezaji hao wote waliotolewa kwa mkopo ni matunda ya Azam FC Academy, ambayo imehusika kutoa nyota kadhaa wanaotamba katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) akiwemo mfungaji bora wa ligi msimu uliopita Simon Msuva anayechezea Yanga.