KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendelea kufanya kweli kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya leo jioni kuichapa Mwadui ya Shinyanga bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Huo ni mchezo wa kwanza wa Azam FC, tokea itoke kuibuka mabingwa wa michuano maalumu iliyomalizika jijini Ndola Zambia, Jumatano iliyopita.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, leo alimwazisha kikosini winga Ramadhan Singano ‘Messi’ akichukua mikoba ya Farid Mussa mwenye majeraha ya kisigino, ambaye alionekana kucheza vema na kuwa kivutio kwa mashabiki waliohudhuria mchezo huo.

Azam FC iliyoanza mchezo huo kwa kasi ikicheza soka safi na la uelewano iliweza kupata bao hilo pekee katika dakika 18 lililofungwa na Kipre Tchetche kwa shuti safi nje kidogo ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa Mwadui, pasi akipokea kutoka kwa Shomari Kapombe.

Bao hilo linamfanya Tchetche kufikisha jumla ya mabao nane ya kufunga kwenye msimamo wa wafungaji bora wa ligi hiyo, na sasa anazidiwa mabao sita tu na vinara Hamis Kiiza (Simba) na Amissi Tambwe (Yanga), waliofunga 14 kila mmoja.

Mabingwa hao wangeweza kuandika mabao zaidi katika kipindi cha kwanza kama mshambuliaji wake, Tchetche angekuwa makini baada ya kukosa takribani mabao manne ya wazi.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Azam FC ilikuwa mbele kwa bao hilo, ambapo katika kipindi cha pili Azam FC bado ilionekana kucheza vema hasa dakika 10 za mwanzo.

Baada ya hapo ilionekana kuzidiwa nguvu na Mwadui na ilirejea mchezoni mara baada ya mabadiliko yaliyofanywa kwa kuingia viungo Frank Domayo na Michael Bolou na hadi dakika 90 zinamalizika Azam FC iliibuka kidedea kwa ushindi huo.

Ushindi huo wa Azam FC, umeifanya izidi kujiongezea rekodi yake ya kuwa timu pekee ambayo mpaka sasa haijafungwa mchezo wowote kwenye mechi 16 za ligi ilizocheza mpaka sasa, ikishinda mechi 13 na kutoa sare tatu ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo kwa pointi 42 sawa na Simba iliyonafasi ya pili.

Lakini Azam FC inazidiwa michezo miwili ya kucheza na Simba, vilevile kwa Yanga pia ambao wapo kileleni wakiwa wamejikusanyia jumla ya pointi 43.

Azam FC itashuka tena dimbani Jumapili ijayo (Februari 14, 2016) kwa kuvaana na Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa;

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika, Pascal Wawa, Jean Mugiraneza, Himid Mao/Kipre Balou dk70, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Frank Domayo dk78, Ramadhan Singano ‘Messi’, Kipre Tchetche/Allan Wanga dk66 na John Bocco.