TIMU ya vijana ya Azam FC ‘Azam FC Academy’, imeendelea kung’ara kwenye mechi zake baada ya kuwachapa vijana wenzao wa Timisemi mabao 6-1 leo mchana.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, ulionekana kuwa mkali sana kutokana na kasi, hasa kipindi cha kwanza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu.

Azam FC Academy ilijipatia mabao hayo kupitia kwa nyota wake, Yohana Mkomola aliyefunga ‘hat trick’, Sadallah Mohamed alipiga mawili huku bao jingine likiwekwa kimiani na Stanislaus Ladislaus.

Mabao hayo yalitosha kabisa kuzima ndoto za Timisemi kutaka kuvuruga rekodi ya Azam FC Academy ya kushinda mechi takribani tano mfululizo tokea mwaka huu uanze, hasa baada ya wao kutangulia kufunga bao hilo kabla ya mvua ya mabao kuwashukia.

Mechi hiyo ilikuwa ni maalumu ya kufungua pazia la mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baina ya Azam FC na Mwadui, ulioisha kwa Azam FC kushinda bao 1-0.