KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo imeendelea kumulika vipaji vipya kwa kutoa nafasi ya majaribio kwa vijana takribani 310 kuonyesha vipaji vyao ili kuweza kujiunga na academy ya timu hiyo.

Programu hiyo iliyosimamiwa na Kocha Mkuu wa Academy ya Azam FC, Tom Legg na Msaidizi wake, Idd Cheche na Kocha wa chini ya miaka 17, John Matambara, ilihusisha vijana takribani 200 waliokuwa wamegawanywa kwenye umri wa chini ya miaka 12 hadi 16, huku 110 wakiwa ni chini ya miaka 20.

Wachezaji hao wote walikuwa wakiangaliwa vipaji walivyokuwa navyo kwa kucheza mechi ndogo ndogo za wenyewe kwa wenyewe na hatimaye benchi la ufundi likavuna takribani 20 ambao wameonyesha uwezo wa kusakata kabumbu.

Miongoni mwa wachezaji hao waliong’amuliwa 17 ni wenye umri wa kuanzia miaka 12 hadi 16 na watatu pekee ndio wameonekana kwa upande wa wale wa chini ya miaka 20.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya majaribio hayo, Kocha Legg alisema huo ni mwendelezo wa programu maalumu waliyojiwekea ya kuangalia vipaji kutoka kwenye jamii kila Jumamosi kwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 12 hadi 16.

“Tumeanza programu za jamii kila Jumamosi, wachezaji mbalimbali wa umri wa miaka 12, 14 na 16 huja hapa kucheza, na sisi huangalia vipaji vyao, tukiona kuna wachezaji wazuri huwaalika tena kuja hapa na kuwapa mafunzo kadhaa na mazoezi ya ziada, tukiona mchezaji yoyote kati ya hao ana mwelekeo mzuri wa kisoka kwa baadaye tutamchukua na kumuingiza katika academy.

“Kwa leo tumepata wachezaji 17 wa umri huo na wengine watatu wa chini ya miaka 20, hawa wa chini ya miaka 20 tutawaita wiki ijayo kwa ajili ya kufanya mazoezi na academy yetu (U-20) na kama watafanya vizuri na hapo tutawachukua,” alisema Legg.

Legg alichukua fursa hiyo kuwakaribisha vijana wote walio chini ya umri wa miaka 20, wenye uwezo wa kucheza soka kutoka kila sehemu ya Tanzania, kuja kwenye viunga vya Azam Complex saa 2.30 asubuhi kwa ajili ya kufanya majaribio katika kila wikiendi ya kwanza ya kila mwezi, ambapo kwa mwezi ujao itakuwa Machi 5, mwaka huu.