KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, mchana wa leo imewachapa mabingwa wa Zimbabwe, Chicken Inn mabao 3-1 katika mchezo wa michuano maalumu inayoendelea kutimua vumbi kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa jijini Ndola, Zambia.

Matokeo hayo yameifanya Azam FC kupanda kileleni kwenye msimamo wa michuano hiyo baada ya kufikisha jumla ya pointi nne sawa na Zanaco FC, lakini ipo juu kwa tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Azam FC iliyoanza michuano hiyo kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji wao Zesco United, iliuanza mchezo huo kwa kujikuta ikitanguliwa kufungwa bao dakika ya 28.

Dakika nne baadaye Azam FC ilijipatia bao safi la kusawazisha lililowekwa kimiani na nahodha wake, John Bocco ‘Adebayor’ na kuufanya mchezo huo kwenda mapumziko kwa sare hiyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kufanya mabadiliko ya kutoka Ame Ally na John Bocco na nafasi zao kuchukuliwa na Allan Wanga pamoja na Kipre Tchetche.

Mabadiliko hayo yalizidi kuiongezea kasi Azam FC hasa eneo la ushambuliaji, ambapo ilifanikiwa kupata penalti dakika ya 54 baada ya Wanga kuangushwa ndani ya eneo la hatari, ambapo alikuwa ni Kipre Tchetche aliyeifunga kiufundi na kuiandikia Azam FC bao la pili.

Azam FC ilizidi kuongeza presha langoni mwa Chicken Inn, ambao mchezaji wao mmoja alijichanganya dakika ya 67 baada ya kujifunga mwenyewe kwa kichwa na kuandika bao la tatu, wakati akimzuia kiungo Frank Domayo asifunge kufuatia kona safi ya Ramadhan Singano ‘Messi’.

Hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika, Azam FC iliondoka na ushindi huo mnono, ambao unaifanya kuwa katika wakati mzuri wa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo katika mechi ya mwisho Jumatano ijayo dhidi ya Zanaco FC ya huko.

Azam FC inahitaji sare au ushindi wowote kuweza kutwaa taji la michuano hiyo, ambayo inafanyika kwa mara ya tatu mfululizo, ambapo TP Mazembe ililitwaa mwaka jana ilipofanyika nchini DR Congo.

Kikosi kilikuwa hivi:

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Ramadhan Singano ‘Messi’, Abdallah Kheri, Pascal Wawa, Himid Mao, Mudathir Yahya, Michael Bolou, Shomari Kapombe/Said Morad dk85, John Bocco/Kipre Tchetche dk46, Ame Ally/Allan Wanga dk46