KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jana jioni ilianza vema kuwania taji la michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuichapa African Lyon mabao 4-0.

Kwa matokeo hayo, Azam FC imefanikiwa kutinga hadi hatua ya 16 bora ya michuano hiyo, ambayo itatoa bingwa atakayeshiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Mchezo huo wa raundi ya tatu uliofanyika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, ulionekana kuwa ni wa upande mmoja hasa kipindi cha kwanza baada ya Azam FC kumiliki sana mpira na kuingia ndani ya eneo la hatari la wapinzani wao kila mara.

Katika mchezo huo Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alikifanyia mabadiliko kadhaa kikosi chake kilichoanza, akiwaanzisha viungo Mudathir Yahya na Michael Bolou huku akimpumzisha Nahodha Msaidizi, Himid Mao ‘Ninja’ na kumabdilisha namba kiungo Jean Mugiraneza ‘Migi’, aliyecheza kama beki wa kati jana akichukua mikoba ya Pascal Wawa ambaya ni majeruhi.

Kasi ya Azam FC kwenye mchezo huo iliwafanya kupata bao la mapema sana, lililofungwa dakika ya 1 na kiungo Mudathir Yahya aliyeunganisha vema pasi ya Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ kwa shuti.

Alikuwa ni winga machachari Farid Mussa dakika mbili baadaye aliyewahadaa mabeki wa African Lyon baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kupiga shuti la kiufundi lililomshinda kipa Hamad Juma na kujaa wavuni akiiandikia Azam FC bao la pili.

Farid alizidi kutakata katika mchezo huo baada ya kutumia vema tena pasi safi ya Sure Boy na kufunga bao jingine bora la mbali dakika ya 37 akimtungua vilivyo kipa Juma, ambaye alikuwa ametoka mbele kidogo kwenye lango lake.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Azam FC iliondoka kifua mbele kwa mabao hayo matatu, kipindi cha pili kilianza kwa kufanya mabadiliko wakimtoa beki Shomari Kapombe na kuingia Khamis Mcha ‘Vialli’.

Kwa kiasi kikubwa mpira ulionekana kubadilika, hasa baada ya African Lyon kuanza kucheza sokana kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Azam FC, ambayo hata hivyo yaliishia kuokolewa na mabeki wa matajiri hao na kipa Aishi Manula.

Azam FC ilipeleka kilio tena kwenye lango la African Lyon baada ya kupata bao la nne lililofungwa na Ame Ally ‘Zungu’ dakika ya 54 akiunganisha pasi safi ya Farid, aliyewatoka mabeki wa kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (VPL).

Kocha Hall alizidi kukifanyia mabadiliko mengine kikosi chake kwa kuwatoa Migi na Bocco na nafasi zao kuchukuliwa na Said Morad pamoja na Allan Wanga, lakini hadi dakika 90 zinamalizika ubao wa matokeo ulibakia kusomeka African Lyon 0-4 Azam FC.

Kocha afunguka

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi, alisema kuwa wamefurahishwa na ushindi mnono walioupata huku akidai kuwa wanakabiliwa na mtihani mgumu zaidi kwenye hatua waliyovuka.

“Mechi haikuwa rahisi, tunamshukuru Mungu kwa kupata ushindi mnono wa mabao manne, katika hatua ijayo tunaweza kupata timu ambayo ni ya Ligi Kuu, hivyo tutahakikisha tunajipanga vema na kuhakikisha tunazidi kufanya vizuri,” alisema.

Katika hatua nyingine alidai kuwa wamefurahishwa na kiwango alichoonyesha Migi kwenye majukumu mapya ya kucheza beki ya kati akichukua mikoba ya Pascal Wawa.

“Tumefurahishwa na kiwango alichoonyesha Migi, amecheza vizuri kama beki wa kati na tuliona anaweza kufanya hivyo mara baada ya kuumia kwa Wawa (Pascal),” alisema.

Azam FC mara baada ya mchezo huo, usiku wa kuamkia leo iliondoka nchini kwa usafiri wa ndege kuelekea jijini Ndola, Zambia kwa ajili ya kushiriki michuano maalum iliyoandaliwa kwa ushirikiano na wenyeji wao, Zesco United na Zanaco.

Mbali na timu hizo tatu zitakazoshiriki michuano hiyo itakayoanza kesho Jumatano hadi Februari 3 mwaka huu, nyingine ni mabingwa wa Zimbabwe Chicken Inn, ambao wataanza kufungua dimba dhidi ya Zanaco siku hiyo saa 8.00 mchana kwa saa za hapa huku Azam FC ikikipiga na Zesco United saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:

Aishi Manula, Shomari Kapombe/Khamis Mcha dk46, Erasto Nyoni, Abdallah Kheri, Jean Mugiraneza/Said Morad dk67, Michael Bolou, Mudathir Yahya, Salum Abubakar, John Bocco/Allan Wanga dk57, Ame Ally, Farid Mussa