BEKI wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Shomari Kapombe, amechochea vita ya ufungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi yake na washambuliaji.

Kapombe amesema kuwa ataendelea kufunga sana mabao kila anapopata nafasi ili kutimiza malengo ya timu yake katika malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

Mpaka sasa ligi ikiwa imemalia mzunguko wa kwanza, beki huyo ameonekana kuwa na kasi kubwa ya kufunga mabao akiwapiku hata washambuliaji akiwa ameshaweka kambani mabao saba.

Idadi hiyo ya mabao hayo imemfanya awakaribie washambuliaji Kipre Tchetche (Azam FC) aliyefunga nane, Elias Maguli (Stand United) na Donald Ngoma (Yanga) waliofunga tisa kila mmoja, Hamis Kiiza (Simba) aliyetupia 10.

Nyota huyo aliyewahi kukipiga AS Cannes ya Ufaransa anakabiliwa na mtihani mwingine wa kumfikia kinara wa ufungaji Amissi Tambwe (Yanga), aliyetupia nyavuni mabao 13 mpaka sasa.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz kuhusu mafanikio yake hayo, Kapombe alisema jambo kubwa linalomfanya kufunga mabao ni juhudi zake binafsi pamoja na mfumo 3-5-2 anaoutumia Kocha Mkuu wao, Stewart Hall.

“Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na mimi kufanikiwa kufunga mabao saba mpaka sasa, lakini kikubwa ninachoweza kusema kwamba pamoja na juhudi lakini ni maelekezo ya mwalimu ambayo nafuata anaponielekeza nini cha kufanya, kwa hiyo ninapofuatilia maelekezo yake kupitia mfumo anaotumia unakuta napata nafasi na kufunga,” alisema.

“Changamoto inayokuja kila mwalimu anakuja na mfumo wake pamoja na falsafa yake, lakini katika mfumo tunaotumia sisi wa 3-5-2, mimi huwa nina kazi mbili uwanjani kwa mujibu wa maelekezo ya kocha kulinda na kushambulia (wingbacks), hivyo nikishambulia ninakuwa kama winga na huwa ninaongeza juhudi ya kufunga mabao,” alisema.

Beki huyo mwenye kasi kubwa uwanjani na krosi hatari pamoja na pasi nzuri za mwisho aliongeza kuwa mabao hayo saba yamemwongezea kitu huku akidai kuwa anahitaji kufunga zaidi kwenye mzunguko wa pili wa ligi,

“Kwa sababu najua nitajitengenezea wasifu mzuri na mkubwa na vilevile nitaendelea kuibeba timu yangu, endapo mimi nitakuwa napata nafasi ya kuendelea kufunga, tutakuwa tutapata matokeo rahisi na kushirikiana na wenzangu kuweza kufunga mabao mengine, lakini vilevile kwa mimi banafsi itakuwa imenitengenezea mazingira ya kuweza kuinuka kimpira zaidi na kuonekana zaidi,” alisema.

Hatalisahau bao alilofunga Nangwanda

Katika hatua nyingine, Kapombe alisema kuwa hataweza kulisahau bao alilofunga dhidi ya Ndanda lililoipa ushindi wa bao 1-0 timu yake, mchezo uliofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

“Kwa kweli mimi nalifurahia sana bao nililofunga dhidi ya Ndanda dakika za mwisho, lilikuwa ni bao muhimu sana kwa timu yangu kwani tuliweza kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo uliokuwa mgumu,” alisema.