TIMU ya vijana ya Azam FC ‘Azam FC Academy’ imezidi kufanya kweli baada ya kuichabanga Vingunguti Combine mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex leo asubuhi.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake kutokana na timu zote mbili kuonyeshana umwamba ndani ya dakika zote 90 na haikuwa kazi rahisi kwa Azam FC Academy kuvuna ushindi huo.

Azam FC Academy ilionyesha wazi kuwa imepania kuibuka kidedea katika mchezo huo kwa kutangulia ufunga bao kupitia kwa Yohana Mkomola kabla ya Shabaan Idd kushindilia msumari wa pili.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo mbili zilitoka uwanjani zikiwa nguvu sawa kwa kufungana mabao mawili kila mmoja.

Mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili na benchi la ufundi la Azam FC Academy chini ya Mwingereza Tom Legg na Msaidizi wake, Idd Cheche, yaliweza kuipatia timu hiyo bao la ushindi kupitia kwa Yahaya.

Ushindi huo ni wa tatu mfululizo kwa kikosi hicho ndani ya mwaka huu baada ya awali kuzichapa Green Warriors (1-0) na mwishoni mwa wiki iliyopita ikaibanjua timu kutoka Dar es Salaam inayojiita African Sports (6-0).